Na.Catherine Sungura,Ikungi
Asilimia 97 ya watoto wanaozaliwa hunyonyeshwa maziwa ya mama, ikiwa asilimia 92 ya watoto hunyonyeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhe. Mwanaidi Khamis wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto kitaifa yanayofanyika kwenye halmashauri ya Ikungi Mkoani Singida.
Mhe. Mwanaidi ameendelea kusema kuwa 43% tu ya watoto  ndio hunyonyeshwa hadi kipindi cha miaka miwili na kuendelea huku takwimu zikionesha 57% tu ya watoto ndiyo hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chakula kingine wala maji ndani ya kipindi cha miezi 6.
 
“Tafiti zinaeleza kuwa mtoto akizaliwa na kuanza kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja kunaweza kuokoa uhai wake kwani kuchelewa kumnyonyesha mtoto kuna changia kwa kiwango kikubwa vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28.” Aliongeza.
Aidha, amesema hapa nchini unyonyeshaji wa watoto wachanga ndani ya saa moja umefikia 90% hivi sasa ikilinganishwa na 54% iliyokuwa mwaka 2018 wakati utoaji wa Vitamini A kwa watoto wa miezi 6-59 nao umeongezeka kutoka 64% mwaka 2018 hadi kufikia 97% hivi sasa.
 
Hata hivyo Naibu Waziri huyo aliwahimiza wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoa huduma kwa wakati husika na kuwaasa wazazi kuendelea kuhudhuria Kliniki kama inavyoagizwa pia wazazi kuwanyonyesha watoto wachanga maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita bila kumlisha chakula kingine wala maji pamoja na kuwanyonyesha watoto kwa kipindi cha miaka miwili na zaidi. 
 
“Kunyonyesha maziwa ya mama kuna faida nyingi kwa mama na mtoto kwa kuwa kunaimarisha afya na ustawi wa mama na mtoto, vilevile unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia aina zote za utapiamlo kwa vile kuna kuwa na uhakika wa chakula kwa watoto wachanga na wadogo”. Alisisitiza
Vile vile amesema ili kuimarisha na kuendeleza juhudi za kulinda Afya ya watoto kupitia unyonyeshaji maziwa ya mama, Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo juu ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama, kuendelea kutenga fedha za kutekeleza afua za kuboresha ulishaji wa watoto ikiwemo elimu ya Afya, lishe na huduma za msingi kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na kutoa miongozo na taarifa sahihi kuhusu unyonyeshaji na namna ya kujikinga na magonjwa hasa ya mlipuko.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Jerry Muro amewataka wakurugenzi na watoa huduma ya Afya wa halmashauri yake kuendelea kutoa elimu juu ya unyonyeshaji na kuwasihi wananchi kuepukana na mimba za utotoni.
 
“Changamoto zinazopelekea wazazi kutonyonyesha watoto zao ni pamoja na mimba za utotoni kwakuwa hawajui umuhimu wa kunyonyesha na wengine kuwa bize na kazi na hivyo kuacha kunyonyesha watoto zao.” Amesema DC Muro
 
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa rai kwa Serikali kuongeza muda wa ruhusa kwa wazazi wanaofanya kazi ili kupata muda mwingi wa kuwanyonyesha watoto zao.
Maadhimisho hayo ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto kitaifa yanayofanyika kwenye halmashauri ya Ikungi Mkoani Singida kuanzia 1-7 Augusti 2022 yenye kauli mbiu isemayo CHUKUA HATUA ENDELEZA UNYONYESHAJI: ELIMISHA NA TOA MSAADA