Na. Damian Kunambi, Njombe

Mahakama kuu kanda ya Iringa iliyokaa kikao chake katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe imewahukumu washtakiwa watatu Elias Jackson Mwenda (31) , Hussein Khamis (31) na Orestus Mbawala(51)kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya James Kaengesa mkazi wa Makambako mkoani Njombe.

Akisoma hukumu hiyo jaji Dk. John Utamwa amesema tukio hilo la mauaji lilitokea mtaa wa Mashujaa uliopo halmashauri ya mji wa Makambako.

Amesema tukio hilo lilitokea mwezi Juni 2016 mnamo saa mbili usiku ambapo marehemu ambaye alikuwa ni dereva wa bodaboda kukodiwa na moja ya washtakiwa hao na alipofika eneo la Mashujaa aliambiwa asimamishe pikipiki na mteja wake huyo.

Imeelezwa kuwa lengo la kumwambia asimame ilikuwa ni makubaliano baina ya washitakiwa hao wote watatu kwamba endapo mwenzao huyo atakodi pikipiki ambayo ni mpya atapaswa kusimama katika eneo hilo hivyo baada ya kusimama walimkaba marehemu na kumnyonga kwa kutumia kamba ambayo waliitengeneza mkoani Njombe na kupora pikipiki

Amesema baada kufanya mauaji hayo walimtupa kwenye shamba la mahindi na kutoweka na pikipiki kuelekea mkoani Mbeya ambapo walikamatwa eneo la Rujewa wakiwa na pikipiki hiyo.

Amesema hukumu imetolewa kwa mujibu wa sheria chini ya kifungu namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Mawakili wa serikali ambao walikuwa upande wa jamhuri na kuwakilishwa na Matiku Nyangero na Andrew Mandwa wameiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu hicho kwakuwa adhabu ya mauaji ya kukusudia ni kunyongwa hadi kufa.

Aidha imeamriwa kuwa Pikipiki iliyokuwa kielelezo cha sita upande wa jamhuri iliyokuwa mali ya marehemu akabidhiwe mke wa marehemu Enelika Nyenzi.

Mawakili upande wa utetezi ambao uliwakilishwa na Musa Mhagama,Byton Kaguo na Octavian Mbungani wamekubaliana na maombi yaliyotolewa na mawakili upande wa serikali.