WAZIRI wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu  Julai 25,2022 amezindua Bodi Mpya ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambapo ameiagiza kuhakikisha inaendelea kufanya kazi kwa weledi.

Akizungumza wakati akizindua Bodi hiyo leo katika Ofisi za MSD Jijini Dar es Salaam amesema bodi hiyo inatakiwa ifanye kazi kuzingatia sheria huku wakisimamia uwekaji wa mifumo mizuri ya usimamizi na usambazaji wa dawa nchini.

Waziri Ummy ameipa jukumu la kuhakikisha inasimamia suala la kupangua safu ya uongozi pamoja na wafanyakazi wa MSD ili utendaji kazi uimarike.

Amesema kuwa MSD ilifanya kazi vizuri na kuaminiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo ameagiza kurudishwa kwa mifumo ya TEHAMA iliyosaidia kudhibiti mianya ya ubadhirifu ndani ya taasisi hiyo.

“Watu wanategemea kuona ufanisi wake,sisi tutawapima bodi kwa utendaji wenu kama dawa zinawafikia wananchi maeneo yanayotakiwa.Ila pia muangalia kama ni kuifumua nyie mtaangalia tunachotaka ni kuona mabadiliko ya kiutendaji ndani ya MSD,”Amesema Waziri Ummy.

Nae Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD), Bi.Rosemary Silaa ameahidi bodi hiyo mpya kuwa bodi hiyo inaanza kazi rasmi ya kuisuka upya MSD.