Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekiri kuwa alikuwa tayari kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wake wa Agosti 9, 2017.

Rais Kenyatta amesema alikuwa tayari kuchukua hatua hiyo kuzuia umwagikaji wa damu ambao ungesababishwa na machafuko ya baada ya uchaguzi.

Kiongozi huyo wa Kenya aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mamia ya viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya katika Ikulu ya Nairobi.

 “Mengi yamesemwa kunihusu. Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa nilitaka kurudi Gatundu baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wangu.

 “Ninathibitisha kwamba madai hayo ni ya kweli. Nilitaka kwenda nyumbani. Ikiwa kujiondoa kwangu kungeleta amani nchini, basi nilikuwa tayari kuondoka. Maisha ya binadamu ni muhimu kuliko wadhifa wa urais,” amasema Rais Kenyatta.

Naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto aliwahi kuwaambia wazee wa Mlima Kenya katika kikao cha faragha kilichofanyika nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi, kuwa nusura ampige kofi Rais Kenyatta alipoonyesha dalili ya kutaka kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mara baada ya ushindi wake kubatilishwa na Mahakama ya Juu.

Katika sauti iliyorekodiwa kisiri kutoka kwenye mkutano huo, Ruto anasikika akisema kuwa, alimlazimisha Rais Kenyatta kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26, 2017.

Wanasiasa wa muungano wa Azimio la Umoja wamekuwa wakitumia ufichuaji huo kumponda William Ruto katika kampeni zao, huku wakijaribu kumfanya Naibu wa Rais aonekane kama kiongozi mwenye uchu wa madaraka.

Alhamisi iliyopita, Ruto alijitetea kuwa hakuwa na nia ya kumpiga kofi Rais Kenyatta kama inavyodaiwa.

Hata hivyo Kenyatta alionekana kumshambulia Ruto kwa ‘kuwapotosha’ Wakenya kuwa “alitaka kuachana na urais ilhali wapinzani wake ndio wamekuwa wakidai kuwa alilenga kubadilisha Katiba kupitia mswada wa BBI ili asalia mamlakani”.

Rais Kenyatta amewataka viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya kutohadaiwa na propaganda za baadhi ya wanasiasa wakati huu Uchaguzi Mkuu unapokaribia.

Uchaguzi wa rais nchini Kenya umepangwa kufanyika Agosti 9 mwaka huu.