Na Kidawa Hamza, Dar
Kushindwa kujiendesha kwa ufanisi kwa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makasha (TICTS) kumesababisha msongamano wa makasha hayo bandari ya Dar es Salaam na kuathiri shughuli muhimu za kiuchumi nchini.

Mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa ni usafirishaji wa zao la parachichi ambapo wafanyabiashara wa zao hilo wanakimbia kusafirisha kupitia bandari ya Dar es Salaam na badala yake hutumia bandari za nchi jirani.

Kusuasua kwa TICTS, kumeongeza gharama ya kusafirisha zao la parachini  nchini na kulikosesha Taifa mapato ya matrilioni ya fedha, kutokana na wafanyabiashara kuikwepa bandari wakikimbilia bandari ya Mombasa, Afrika Kusini na Namibia zenye ufanisi zaidi.

Kutokana na udhaifu wa TICTS, gharama za kuhudumia shehena na makasha zinazopita bandarini zimeongezeka na hivyo kufanya wawekezaji ambao walikua na nia ya kuja kuweza nchi kughahiri na kwenda nchi nyingine.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa uzalishaji wa parachichi ikitanguliwa na Afrika Kusini na Kenya, lakini inaweza kuwa ya kwanza endapo mageuzi yatafanyika na kuipa tenda kampuni nyingine itakayo fanya kazi kwa ufanisi bandarini ili kuwapa ari wakulima kulima kwa wingi zao hilo.