Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya operesheni, misako na doria mbalimbali hali inayopelekea Amani na Utulivu kwa raia na mali zao ndani ya Mkoa wetu. Katika misako na doria zilizofanyika hivi karibuni tumepata mafanikio kama ifuatavyo:-

WATATU WATIWA MBARONI KWA KOSA LA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.

Mnamo tarehe 02 Julai, 2022 majira ya saa 09:40 Alasiri, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa Wanyamapori lilifanya msako huko Mtaa wa Mbalizi Msikitini katika Mji Mdogo wa Mbalizi, Mkoa wa Mbeya baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na vipande kumi vya meno ya Tembo.

Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na:-

  1. RASHID JUMA MWAJANGA [33] Mkazi wa Lupa – Chunya.
  2. JUMA FIDELIS MTENGA [42] Mkazi wa Mbuyuni – Songwe.
  3. COSMAS SIMON RANWELU [25] Mkazi wa Lupa – Chunya.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                      

Vipande hivyo kumi vya meno ya Tembo vina jumla ya kilogramu 7.1 na thamani ya Tshs 69,477,300/= sawa na Tembo wawili. Watuhumiwa walikamatwa na kufanyiwa upekuzi kwa mujibu wa sheria na kukutwa na nyara hizo za serikali wakiwa wamehifadhi kwenye mifuko mitatu ya Salfet na kisha kuweka kwenye begi dogo jeusi.

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

KUKAMATWA KWA MTANDAO WA WIZI WA MAGARI JIJINI MBEYA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendesha misako katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya dhidi ya wahalifu wa makosa ya wizi wa Magari na Pikipiki na katika misako hiyo watuhumiwa watatu wanaojihusisha na wizi wa magari wamekamatwa pamoja na magari manne ya wizi.

Watuhumiwa waliokamatwa ni:-

  1. YUSUPH OMARY RAMADHAN [26] Mkazi wa Forest Jijini Mbeya.
  2. SHUKU JOSEPH NYEMA [23] Mkazi wa Songea Mkoa wa Ruvuma.
  3. ABUU NOELY RUTAGALAMA [26] Mkazi wa Itezi Jijini Mbeya.

Aidha katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria watuhumiwa wamekutwa na magari mengine manne ambayo wamekiri ni ya wizi ambayo ni:-

  1. T.786 DLD TOYOTA IST. 
  2. T.649 DMH TOYOTA IST. 
  3. TOYOTA IST isiyo na namba za usajili, 
  4. 4. TOYOTA SPACIO isiyo na namba za usajili.

Aidha watuhumiwa wamekiri kuhusika katika tukio la tarehe 06.04.2022 ambapo waliiba Gari aina ya TOYOTA PRADO TX lenye namba za usajili. T.795 DES mali ya GEDION MAPUNDA Uyole – Jijini Mbeya. Sambamba na hilo watuhumiwa wamekiri kujihusisha na matukio ya wizi wa magari mikoa ya Dar es Salaam na Njombe. 

TAARIFA YA KIFO.

Mnamo tarehe 04.07.2022 majira ya saa 02:00 usiku huko Block T, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, FRANCIS KIRONGO [23] Mwendesha Pikipiki @ Bodaboda alikutwa akiwa ameuawa kwa kupigwa kitu butu usoni na kichwani na mtu/watu wasiofahamika na kisha kuporwa Pikipiki yake MC.861 DCJ Haojue. 

Ni kwamba siku hiyo ya tukio marehemu akiwa maeneo ya Uyole – Kijiwe cha bodaboda cha Bar ya Universal alikodiwa na abiria wawili na kuondoka nao akiwa na Pikipiki yake aina ya Haojue yenye Na. MC.861 DCJ na baada ya hapo hakuonekana tena mpaka alipokutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa chooni. Chanzo cha tukio hili ni kuwania mali.

Kufuatia tukio hilo, ufuatiliaji ulifanyika ndipo mnamo tarehe 05.07.2022 majira ya saa 08:40 mchana huko Nsalaga mmoja wa Bodaboda katika kijiwe cha marehemu [Universal Bar] alimuona na kumtambua mmoja wa abiria aliyemkodi marehemu, alitoa taarifa kwa bodaboda wenzake wakajikusanya na kumzingira mtu huyo akiwa na wenzake wote wa kiume umri kati ya miaka 25-30 kwa majina bado hawajafahamika wakashambuliwa na kufariki wakiwa wanapelekwa Hospitali kwa matibabu. Aidha walikutwa na Pikipiki nyingine yenye namba za usaji MC.864 DHF aina ya Kinglion ambayo ilitambuliwa baadae kuwa ni mali ya PIUS KABUNGA [22] Mkazi wa Igurusi Wilaya ya Mbarali aliyenyang’anywa baada ya kutishiwa Panga na watu hao waliouawa. Chanzo cha tukio hili ni tuhuma za mauaji na wizi wa Pikipiki. Miili ya Marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Igawilo kwa Uchunguzi wa kitabibu na utambuzi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa shukrani za dhati kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kwa ushirikiano wanaoutoa hasa katika mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa rai kwa madereva Bodaboda kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi kwa ajili ya kujilinda katika vijiwe vyao. Sambamba na hilo tunaendelea kutoa wito kwa watendaji wa kata kushirikiana na wakaguzi wa Kata waliopo katika maeneo yao ili kuzuia uhalifu.

Imetolewa na,

ULRICH O. MATEI – SACP

Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Mbeya.