Syria imetangaza leo kuwa inakata uhusiano wake na Ukraine na badala yake kumuunga mkono mshirika wake wa karibu Urusi, ikisema hatua hiyo ni jibu kwa serikali ya mjini Kyiv baada ya Ukraine kuchukua hatua sawa na hiyo. 

Afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Syria ambaye hakutambuliwa kwa jina, ameliambia shirika la habari la serikali la SANA kuwa Jamhuri hiyo ya Kiarabu ya Syria imeamua kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine kwa kuzingatia kanuni za usawa na kujibu uamuzi wa serikali ya Ukraine. 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mwishoni mwa mwezi uliopita alitangaza kuvunja uhusiano wao na Syria baada ya rais wa Syria Bashar al-Assad kuyatambua kama jamhuri maeneo yanayotaka kujitenga ya Donetsk na Lugansk mashariki mwa Ukraine na ambayo yanaungwa mkono na Urusi. 

Majimbo yaliyojitenga ya Donetsk na Lugansk, ambayo uhuru wao ulitambuliwa na Urusi mwezi Februari, yako katika mkoa wa Donbas ambao umeshuhudia mashambulizi makali kutoka kwa vikosi vya Urusi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 24.