Na Eleuteri Mangi, WUSM, Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Seikali sikivu, toeni maoni yenu Serikali itayafanyia kazi ili kuboresha sekta ya Sanaa nchini hatua inayosaidia kuwa na namna bora ya kukusanya na kutoa mirabaha kwa wasanii ndani ya robo mwaka 2022/2023.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe, Pauline Gekul amesema hayo Julai 19, 2022 jijini Arusha alipokuwa akiongea na wasanaii kutoka mikoa ya Arusha, Tanga na Kilimanjaro wakati wakitoa maoni yao mbele ya Kamati ya Kuratibu na Kusimamia Hakimiliki kwa Wasanii ambao wanakukusanya maoni ya wasanii hatua inayosaidia Serikali kuboresha ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha kwa wasanii nchini.

“Wewe ndiye unafahamu nini kiboreshwe zaidi, sisi Serikali tunapokea maoni yenu sisi tutayafanyia kazi, nimewaomba wajumbe wa kamati wawe wavumilivu, wapokee maoni na yale yasiyo ya mirabaha watuletee kwa sababu tumeamua kuondoa malalamiko kwenye sekta hii ya Sanaa” amesema Naibu Waziri Gekul.

Aidha, Naibu Waziri Gekul amewaagiza Maafisa Utamaduni kote nchini kupitia mikoa, wilaya na hamashauri wakae na wasanii kwenye maeneo yao wasisubiri kamati inayokusanya maoni hatua inayosaidia kuongeza wigo wa kukusanya maoni ili wasanii wa muziki, wachongaji, wachoraji, wabunifu, waigizaji, waandishi waweze kunufaika na kazi zao.

Kwa kuwajali wasanii nchini, Naibu Waziri Gekul amesema Serikali kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga kiasi cha Sh. 2,000,000,000 ambapo moja ya majukumu yake ni kutoa elimu kwa wasanii inayoendana na maadili ya Kitanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu na Kusimamia Hakimiliki kwa Wasanii inayoendelea kukusanya maoni ya wadau kupata namna bora ya kuboresha ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha Bw. Victor Tesha amesema Serikali imesikia kilio cha wasanii cha muda mrefu na imeunda kamati hiyo ili iweze kupata maoni na kuyafanyia kazi hatua itakayosaidia kupata njia bora ya kuwapatia wasanii haki zao.