TUME ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) imemteua, Tamima Haji Abass kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya uteuzi huo kufuatia kikao chake cha Julai 9, 2022 kwa kuzingatia matakwa ya ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A (6) na (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa Julai 9, 2022 na Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dkt.Wilson Mahera Charles.
Amesema, uteuzi huo umefanyika baada ya tume hiyo kupkea barua Mei 12, 2022 yenye Kumb. Na. CEB. 137/400/02A/10 kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoandikwa kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Barua hiyo ilitaarifu kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama.