Na Mary Gwera, Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa wito kwa wananchi hususani wanaume kuandika wosia ili kuepusha migogoro mbalimbali ikiwemo ya kugombea mali kwa familia wanazoziacha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijni Dar es Salaam  tarehe 08 Julai, 2022 alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania lililopo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa familia nyingi hususani wajane na watoto wamekuwa wakikabiliana na migogoro ya kugombea mali zilizoachwa na marehemu.

“Wajane wengi wanakabiliwa na migogoro kutoka kwa ndugu pindi mume anapofariki, hivyo ni rai yangu kwa Watanzania na haswa wanaume wenzangu kuandika wosia ili kuepusha matatizo yanayotokea kwa mjane na Watoto,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa katika jitihada za kuhakikisha kuwa Mahakama inashughulikia kwa ukaribu masuala ya familia ikiwemo Mirathi, Mahakama ilianzisha kituo maalum cha kushughulikia masuala ya familia hivyo kuwataka wananchi kutosita kupata huduma zinazotolewa katika kituo hicho.

Aidha; Mtendaji Mkuu amesema katika kipindi cha Maonesho ya ‘sabasaba’ moja ya huduma zinazotolewa katika banda la Mahakama ni pamoja na kutoa elimu ya Wosia na Mirathi hivyo ni vyema wananchi watembelee banda hilo ili kujua zaidi.

Kwa upande mwingine, Mtendaji Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuendelea kutumia namba ya huduma kwa mteja ya Mahakama ‘Call Centre’ ambayo ni 0752 500 400 ili kupata utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowasibu kuhusu Mahakama.

“Tumeanzisha hii ‘call centre’ maalum kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, unapokutana changamoto yoyote usimpigie Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi au Msajili Mkuu bali piga namba 0752 500 400 inayopatikana masaa 24,” amesema Mtendaji Mkuu.

Mahakama ya Tanzania ni moja ya Taasisi zinazoshiriki katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa lengo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na huduma inazotoa.