Watu watano wamefariki dunia na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya lori la mizigo lililobeba shehena ya mahindi kufeli breki na kugonga badi dogo la abiria aina ya Coaster liliyokuwa likitoka Mbeya mjini kwenda Wilaya ya Mbarali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amesema kuwa ajali hiyo imetokea  Jumanne Julai 5, 2022 kwenye mteremko mkali wa barabara kuu ya Mbeya-Dar es Salaam

Kamanda Matei amesema kuwa lori la mizigo lililokuwa tela liligonga gari la abiria na kisha kuliburuza mpaka kwenye vibanda vilivyopo pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

 ''Gari lililosababisha ajali lilitokea Mkoa wa Songwe kwenda jijini Dar es Salaam huku likiwa limebeba shehena za mahindi na chanzo cha ajali ni kufeli breki kutokana na mteremko mkali ambao alishindwa kulimudu'' amesema

Matei amesema miili ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo imehifadhiwa kwenye kituo cha afya cha Inyala huku majeruhi  wakipelekwa Hosptali ya Wilaya ya Igawilo ya Mbeya ambapo idadi yao bado haijafahamika.

Kamanda Matei amesema kuwa hiyo ni ajali ya pili kutokea kwenye eneo hilo kwa siku za hivi karibuni, ambapo June mwaka huu magari manne yaligongana huku mawili yakiteketea kwa moto na kusababisha kifo cha mtu mmoja.