Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bwana Honest Njau ameuzungumzia mradi huo kuwa ni mradi wa kimapinduzi unaoenda kuboresha na kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za uzalishaji pamoja na kutoa au kupokea huduma za Serikali na zile za kijamii na kiuchumi

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara hiyo yanayofanyika jijini Arusha, Bwana Njau amesema kuwa ili kuweza kuwa na mabalozi wazuri ni vema kila mtumishi kufahamu kinachoenda kufanyika kupitia mradi huo ili kufikia uchumi wa kidijitali

“Tayari tupo kwenye zama za kidijitali, kinachofanyika kupitia mradi huu ni kuboresha zaidi kwa kuchangia kuongeza wigo wa kutoa huduma za Serikali kwa wananchi, kuboresha huduma za mawasiliano na kuhakikisha Taifa linakuwa na wataalamu weledi na wabunifu wa kutosha wa TEHAMA ili kuweza kusimamia mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea kufanyika nchini na duniani kote”, amezungumza Njau

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo Serikali inakwenda kuboresha miundombinu na maeneo mahususi ya uchumi ili kuendana na uchumi wa Kidijitali ikiwa ni pamoja na kuwezesha biashara mtandao kwa kutengeneza platform kubwa ya biashara itakayoiunganisha nchi na dunia

“Tunaposema majukwaa(platforms) ya biashara mtandao haimaanishi mitandao ya kijamii pekee ila ni pamoja na kuwa na majukwaa mengine ya kufanya biashara mtandao kwa mfano Sarafu ya Azam Bakhresa, Alibaba, Kikuu na mingine mingi kama hiyo, hivyo kama nchi tunatakiwa kuwa na platform kubwa itakayotuunganisha na dunia”, amefafanua Njau

Katika hatua nyingine, watumishi hao wamepitishwa katika mada ya matumizi salama ya mtandao ambapo, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Usalama Mtandao wa Wizara hiyo, Mhandisi Steven Wangwe aliyetoa mada hiyo kwa njia ya mtandao ameangazia sheria yenyewe ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na makosa yake yanayoweza kutokea kwa kukiuka usiri, uadilifu na upatikanaji wa taarifa.

Mhandisi Wangwe ameyabainisha makosa yanayofanyika kwa njia ya mtandao ni pamoja na usambazaji wa taarifa isivyo kwa usahihi, udhalilishaji wa mtandao, kutoa taarifa za uongo, utapeli kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta, usambazaji wa picha za utupu na faragha kwenye mitandao, kutuma barua pepe au meseji za vitisho pamoja na udukuzi wa taarifa.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kunakuwa na matumizi salama ya mtandao kwa kutunga na kusimamia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 inayoainisha makosa ya kimtandao na adhabu zake ambazo ni pamoja na faini, kifungo au vyote kwa pamoja kulingana na aina ya kosa husika.