Urusi imefyatua makombora kadhaa na kuvilenga vituo vya kijeshi katika maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Ukraine leo, wakati mzozo huo mkubwa barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia ukiingia mwezi wake wa tano.

Gavana wa mkoa wa Lviv ulioko magharibi mwa Ukraine, Maxim Kozytskyi amesema kuwa makombora yapatayo sita yamefyatuliwa kutokea bahari nyeusi dhidi ya kambi ya kijeshi ya Yavoriv. 

Makombora mengine takribani 30 yalirushwa dhidi ya kituo cha kijeshi kimoja karibu na mji wa Zhytomyr. Miji pacha ya Sievierodonetsk na Lysychansk nayo imeshambuliwa kwa mizinga mapema hii leo na kukipiga kiwanda cha kemikali ambako mamia ya raia walikuwa wamekwama.

Ukraine ilitangaza siku ya Ijumaa kuviondoa vikosi vyake katika mji wa Sieverodonetsk, ili kuepusha kuzingirwa na vikosi vya Urusi.