Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekamilisha majadiliano ya mkataba wa kuondoa utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili.
Nyaraka za kufikiwa kwa majadiliano hayo zimetiwa Saini jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mheshimiwa Khalifa Abdulrahman Almarzooqi na Bw. Abdullah Ahmed Al Obaidali, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Mashirika ya Fedha.
Bw. Mafuru alieleza kuwa makubaliano hayo yatakayofuatiwa na utiaji Saini mikataba yake muda si mrefu yanafuatia jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozifanya hivi karibuni katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo aliagiza kuondolewa kwa changamoto hiyo ili kukuza mahusiano ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya uwekezaji.
“Ni matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu kukamilika tutaona uwekezaji mkubwa ukija baina ya nchi zetu hizi na hasa kutoka Uarabuni ambao wana mitaji mikubwa lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza, hata wawekezaji, wafanyabiashara wa Tanzania wataweza kufanya biashara bila kuwa na mashaka ya kutozwa kodi mara mbili hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili” alisema Bw. Mafuru.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mheshimiwa Khalifa Abdulrahman Almarzooqi alisema kuwa hatua iliyofikiwa ya kuondoa utozaji kodi ya mapato mara mbili kati ya Tanzania na UAE kutavutia wawekezaji wengi aidi kutoka katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Alipongeza jitihada zinazofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kufanikisha jambo hilo la kuondoa utozaji wa kodi ya mapato mara mbili na kwamba hatua hiyo itavutia mitaji na wawekezaji wengi kutoka nchi za Kiarabu kuja kuwekeza Tanzania.