Na Mwandishi Wetu, ARUSHA

Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) lenye ghorofa 18 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 39, jijini Arusha inadhihirisha kuwa Tanzania inastahili kuwa makao makuu ya umoja huo na kuwa kitovu cha Sekta ya Posta kwa Bara la Afrika

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi Caroline Kanuti alipozungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara hiyo waliofika kuona maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo siku ya jumatano ya Juni 8, 2022, jijini Arusha

Bi. Kanuti amesema kuwa kufanikisha ujenzi wa Makao Makuu ya PAPU jijini Arusha ni fahari kwa nchi ya Tanzania kwa kuwa imedhihirisha inastahili na ina sifa ya kuwa mwenyeji wa makao makuu ya umoja huo lakini pia itaifanya nchi ya Tanzania kuwa kitovu cha shughuli zote za Sekta ya Posta Barani Afrika

Ameongeza kuwa asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo zinatoka kwa nchi 45 wanachama wa PAPU na Tanzania ikiwemo, na asilimia 40 ya gharama za ujenzi huo zinatoka Serikalini kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ndio msimamizi wa Sekta ya Posta nchini

“Jengo hili ni ofisi lakini pia ni kitega uchumi cha nchi wanachama wa PAPU, na faida itakayopatikana itagawanywa kulingana na makubaliano yaliyoingiwa na umoja huo ambapo asilimia 60 itaenda kwa PAPU na asilimia 40 kwa Serikali ya Tanzania”, amezungumza Kanuti

Msimamizi wa ujenzi wa jengo la ofisi za PAPU, Arusha, Mhandisi Hanington Kagiraki amesema jengo hilo linajengwa kisasa na kwa ubora wa hali ya juu ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 70 na matumizi ya rasilimali fedha ni asilimia 51

Ameongeza kuwa, matumizi ya jengo hilo mbali na ofisi za PAPU, kutakuwa na ofisi ya TCRA Kanda ya Kaskazini, ofisi ya Shirika la Posta Tanzania, kumbi za mikutano, ofisi za kukodisha, sehemu ya kulia chakula (restaurants), sehemu maalumu kwa ajili ya chakula cha Kiswahili na juu kabisa ghorofa ya 18 litakuwa ni eneo la watalii kutazama vivutio vya jiji la Arusha

Naye Katibu Mkuu Mtendaji wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Bwana Sifundo Chief Moyo amesema kuwa nchi ya Tanzania inatakiwa kuona fahari kuwa mwenyeji na mwanachama wa umoja huo na yeye binafsi anafurahia uwepo wa Makao Makuu ya Umoja huo nchini kwa kuwa nchi ya Tanzania imedhihirisha kuwa kituo cha Jumuiya nyingi za kiafrika

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-MAELEZO wa Wizara hiyo, Rodney Thadeus, amesema kuwa kuna faida nyingi zitapatikana kwa nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa taasisi kubwa barani Afrika kwa kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi wa jiji la Arusha na nchi kwa ujumla kupitia mikutano ya kimataifa na shughuli nyingine za kiuchumi zitakazofanyika katika jengo hilo