Na Lucas Raphael-Tabora
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha sh bil 15 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuimarisha shughuli za vyama vya ushirika nchini na kuinua wakulima.
Hayo yamebainishwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) ambayo yanafanyika Kitaifa katika viwanja vya Nane Nane vilivyoko Ipuli Mjini Tabora.
Alisema dhamira ya serikali ni kuinua vyama vya ushirika na kukuza sekta ya kilimo kutoka asilimia 4 ya sasa hadi 8 na kufikisha asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 lengo likiwa kupanua wigo wa uzalishaji ili kumnufaisha zaidi mkulima.
Alibainisha kuwa ili kufanikisha lengo hilo serikali imeongeza bajeti kuu ya Wizara hiyo kutoka sh bil 294 hadi bil 954 huku bajeti ya kuinua ushirika pekee ikiongezeka kutoka sh bil 12 hadi 15 katika mwaka huu wa fedha.
Naibu Waziri aliongeza kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo inavutia wadau wengi zaidi ikiwemo kukuza uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla, kupunguza umaskini, kutengeneza ajira na kuanzishwa mashamba makubwa (block farm10,000 ).
Alisisitiza kuwa ushirika ni nyenzo muhimu sana hivyo akamtaka Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika kuelimisha jamii juu ya manufaa ya ushirika ili usiharibiwe kuondoa dhana hasi miongoni mwa watu juu.
‘Naipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini kwa kazi nzuri mnayofanya kusimamia na kuelimisha jamii juu ya manufaa ya kujiunga kwenye ushirika’, alisema.
Aliongeza mikakati mingine ya Wizara hiyo kuwa ni kuongeza uzalishaji wa mbegu ambapo wanatarajia kutumia kiasi cha sh bil 43, kuboresha miradi ya umwagiliaji kwa sh bil 361 na kuhifadhi mazao ya wakulima.
Mavunde alielekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) na Chuo Kikuu cha Ushirika (MUCCOBS) kuendelea kutoa mafunzo ya usimamizi vyama vya ushirika, utunzaji nyaraka na uendeshaji shughuli zao ili kuwaongezea ufanisi.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa wilaya ya Tabora Dkt Yahaya Nawanda alisisistiza kuwa wataendelea kuhimiza uanzishwaji vyama vya ushirika kutokana na umuhimu wake kwa jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani hapa Hassan Wakasuvi alipongeza serikali kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa vitendo katika kuimarisha ushirika hapa nchini ili kuwainua wakulima.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege alibainisha kuwa maadhimisho hayo ni muhimu sana kwani wanaushirika watapata fursa ya kuonesha kazi zao na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wenzao.