Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amekutana na kufanya mazungumzo na makamu wa Rais na meneja mkuu wa Paramount Africa and Peer Lead BET International, Monde Twala,  na kukubaliana kushirikiana katika kuiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa tuzo za MAMA- MTV Africa Music Award kwa mwaka 2023.
 
Waziri Mchengerwa amekutana na Monde Twala Jijini Los Angeles   katika jimbo la California nchini Marekani wakati wa hafla ya utoaji tuzo za BET kwa mwaka 2022.
 
Katika mazungumzo hayo Waziri Mchengerwa amemwelezea nia na sababu ya Tanzania kutaka kuwa mwenyeji wa tamasha hilo la utoaji wa tuzo hizo kubwa za burudani kwa Afrika, kuwa ni kuongeza ushawishi kwa vijana wa kitanzania kuendelea kufanya vizuri katika sekta za burudani Pamoja na kuitangaza zaidi Tanzania na uzuri wake katika ulimwengu.
 
Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimekubaliana  kuungana kwenye kutafuta washirika katika kuendesha tuzo hizo, na kuridhia kuwa maandalizi yaanze mara moja, huku wakipendekeza muda wa tamasha hilo la utoaji tuzo kufanyika mwezi Octoba 2023 jijini Dar Es Salaam.
 
 “Tuna kila sababu ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za MAMA- MTV  African Music Awards kwa mwaka 2023 kwa sababu lengo letu ni kuitangaza nchi yetu zaidi na katika hili lazima tufanikiwe, kwa sababu hakuna kinacho shindikana, tuna kila kitu na ninaamini tunaweza” alisema Waziri Mchengerwa.
 
Kwa upande wake Tawala amesema anaiona Tanzania kama eneo lenye vipaji vya hali ya juu katika sekta ya Sanaa, na burudani ambavyo havijaonekana na kutumika kwa manufaa ya nchi na manufaa ya wasanii wenyewe, na kuahidi kushiriki moja kwa moja katika kuwezesha kufanyika kwa tuzo hizo nchini Tanzania kwa mwaka 2023.
 
Katika ziara hiyo Waziri Mchenegerwa ameambatana na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi pamoja na Mkurugenzi wa Sanaa dkt. Emmanuel Ishengoma ambao wapo nchini marekani, kutafuta uzoefu wa namna ya kuandaa tuzo kwa kiwango cha kimataifa, lengo likiwa ni kuunga mkono juhudu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia washiriki wa moja kwa moja na mamilioni watakao fuatilia mubashara tamasha la utoaji wa tuzo hizo.
 
Wakiwa Nchini Marekeni wameudhuria tamasha la utoaji wa tuzo za BET kwa mwaka 2022, lililofanyika June 26 katika ukumbi wa burudani (arena) wa Microsoft theater, tuzo ambazo ni za kimataifa zinazotolewa mara moja kwa mwaka kama sehemu ya kusherehekea mafaniko ya wamarekani weusi katika muziki, maigizo na michezo.
 
Viongozi hao pia wanatarajia kutembelea kampuni mbalimbali za uzalishaji wa filamu na muziki, lengo likiwa ni kutengeneza mahusiano na kuona namna Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inavyoweza kuwawezesha wataalamu kutoka katika makapuni hayo maarufu duniani kuwajengea uwezo wazalishaji wa muziki na filamu wa hapa nchini Tanzania.