Wizara ya maji imetangaza Rasmi Bei elekezi za Gharama za Maji vijijini na kufanya uchambuzi wa Bei za Maji kwenye Vyombo vya watoa huduma za Maji ngazi ya Jamii na kuzionya jumuiya za maji kuzingatia maelekezo hayo kwani haitawafumbia macho watakaokwenda kinyume.
Waziri wa Maji Juma Aweso ameziweka wazi bei za kikomo kwa ndoo ya lita 20 kama ifuatavyo ikiendana na mifumo/nishati inayotumika kusukuma Maji ambapo Mfumo wa Nishati ya mafuta ndoo ya lita 20 ni shillingi 50, Mfumo/Nishati ya Umeme Jua shillingi 30, Mserereko Shillingi 20 Umeme wa Tanesco shillingi 40 na Pampu za mkono Bei iwe shillingi 20.
Amesema Bei za Ukomo kwa mita ya ujazo itakua shillingi 2,500/= kutoka shillingi 5,000/= ilivyokua na hivyo Bei za ukomo kwa ndoo ya lita 20 itakua shillingi 50 badala ya shillingi 100 ya awali.
Awali amesisitiza kuwa hii ni dhamira ya dhati ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kazi ya Wizara ni kutekeleza maono hayo kwa kuwapunguzia mzigo wanancho vijijini.
Pia Aweso ametoa vifaa vitakavyotumika katika utendaji kazi ikiwa ni pikipiki 250 kuongeza kwenye 145 zilizokwisha kugawiwa awali mwaka jana ikiwa ni jumla ya 395 kwenda kuboresha utendaji kazi, ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wa majukumu sekta ya maji vijijini.