Putin aionya Ukraine isijaribu kumiliki makombora ya masafa marefu
Rais Vladimir Putin wa Russia ameionya Ukraine kuwa itakabiliwa na mashambulio makali zaidi iwapo itathubutu kupokea makombora ya masafa marefu kutoka nchi za Magharibi.
Akiungumza katika mahojiano na Televisheni ya Russia 1 leo Jumapili, Rais Putin ameashiria uwezekano wa Ukraine kupokea makombora ya masafa marefu na kusema: "Iwapo itakabidhiwa makombora hayo, basi tutatumia silaha zetu, ambazo tunazo za kutosha, na tutalenga maeneo ambayo hadi sasa hatujayalenga."
Rais wa Russia aidha amesema uamuzi wa Marekani wa kutuma mfumo wa kuvurumisha makombora kadhaa mara moja ambao Rais Joe Biden aliahidi kuikabidhi Ukraine hautaleta chochote kipya kwa askari wa Kiev. Amesema silaha hizo hazina maana kwani hivi sasa jeshi la Ukraine lina mifumo sawa na hiyo ya makombora aina ya Grad, Smerch, na Uragan ambayo imekuwa ikiimiliki tokea zama za Sovieti.
Hayo yanajiri wakati ambao mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amekiri kuwa, vita nchini Ukraine vimeleta mgogoro wa chakula katika kila kona ya dunia lakini wakati huo huo nchi za umoja huo na Marekani zinaendelea kuchochea vita hivyo na kuisheheneza silaha Ukraine.