Odinga na Ruto waidhinishwa kugombea urais wa Kenya
Mgombea kiti cha urais wa Kenya kwa tikiti ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga, leo ameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi IEBC kugombea urais katika uchaguzi wa Agosti 9 siku moja baada ya hasimu wake mkuu, William Ruto nae pia kudhinishwa na tume hiyo.
Mapema leo Odinga alifika mbele ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika Ukumbi wa Bomas na kuwasilisha makaratsi yake na baada ya kukaguliwa ameidhinishwa kugombea urais.
Mgombea mwenza wake, Bi. Martha Karua, wa chama cha NARC-Kenya, naye pia amepitishwa kuwania nafasi ya Naibu wa Rais kwa tikiti ya Muungano wa Azimio.
Hii itakuwa ni mara ya tano mfululizo ambapo Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 77, anagombea urais.
Aliwahi kugomeba urais bila mafanikio katika chaguzi zilizofanyika 1997, 2007, 2013 na 2017. Martha Karua, 64, naye aligombea urasi mwaka 2013 bila mafanikio na mara hii anajaribu bahati yake kama mgombea mwenza.
Iwapo Odinga atashinda katika uchaguzi wa Agosti, hii itakuwa mara ya kwanza Kenya kuwa na makamu au naibu rais mwanamke.
Mara hii Odinga anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta kufuatia mapatano ya wawili hao Machi 2018 maarufu kama handisheki na ana matumaini makubwa kuwa uungaji mkono wa serikali iliyopo madarakni utamuwezesha kushinda. Mapatano hayo ya Odinga na Kenyatta yalipelekea kutengwa Naibu Rais William Ruto katika shughuli za kiserikali.
Jana IEBC ilimuidhinisha Ruto na mgombea mwenza wake Righathi Gachagua kuwani urais. Hii ni mara ya kwanza kwa Ruto, 55, kuwania urais ambapo anajaribu bahati yake kupitia Muungano wa Kenya Kwanza.