Mawakili wa upande wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wameiomba mahakama ya hakimu mkazi Moshi kuahirisha kesi hiyo ili Sabaya apelekwe hospitali kutibiwa kutokana na uvimbe alionao kichwani.

Ombi hilo limetolewa hii leo na Wakili Hellen Mahuna mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Salome Mshasha.

Wakili Hellen amedai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa namba moja ambaye ni Sabaya ni mgonjwa na anatakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji.

Amedai mshtakiwa huyo alipata uvimbe huo akiwa kazini, hivyo Mawakili wanaomba kesi hiyo iahirishwe ili akafanyiwe upasuaji.

Mahakama hiyo ya hakimu mkazi Moshi imeahirisha kesi hiyo ya
uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya na wenzake wanne hadi Juni 20 mwaka huu
.