MKAZI wa Maswa Mkoani Simiyu, Salum Nkonja maarufu kama Emmanuel Mkonja , amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi akikabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi yenye mashitaka 11 yakiwemo ya kukutwa na sehemu za siri za mwanamke na nyara za serikali. 

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Caroline Matemu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Ramadhani Rugemalila imedai mshtakiwa alikutwa na kosa hilo Oktoba 30, mwaka 2017, katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam,.

Inadaiwa katika shtaka la kwanza hadi la nane kati ya Oktoba 30 na Novemba 30, 2017 huko bungo, Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki nyara za serikali zenye thamani ya Jumla ya Sh 20,536,555.

Amezitaja nyara hizo kuwa ni uume wa Mbwamwitu wenye thamani ya sh 2,272,600, uume wa Nyumbu wenye thamani ya sh 1,477,450, mikia mitano ya ngiri yenye thamani ya sh 5,114,250 na uume wa fisi mitatu, yenye thamani ya sh 3,750,450.

Pia alikutwa akimiliki yai moja la Mbuni lénye thamani ya sh 2,827,600, ngozi moja iliyokaushwa ndege aina ya Ngekewa mwenye thamani ya sh 227,300 na kichwa kimoja cha nyoka aina ya Kobra chenye thamani ya sh 193,205.

Pia mshtakiwa Mkonje anadaiwa kukutwa akimiliki viungo vya binadamu ambavyo ni sehemu za siri za mwanamke tano, mafuvu mawili ya binadamu na chuchu tano za mwanamke.

Hata hivyo mshtakiwa amekana kukutwa na viungo hivyo na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalimtaka kuwa na wadhamini wawili waliopaswa kusaini bondi ya Sh. Milioni tano.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umeishakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julia 5, 2022 itakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kesi kuanza kusikilizwa.