Majeshi ya Sudan yalifyatua mizinga mikubwa wakati wa mapigano katika eneo la mashariki linalozozaniwa la al-Fashaqa linalopakana na Ethiopia.

Hayo yamedokezwa na afisa wa Ethiopia huku kukiwa na wasiwasi wa kuibuka tena mvutano baina ya nchi hizo mbili kuhusu  mzozo wa muda mrefu katika eneo hilo la mpaka wa pamoja.

Jumanne Sudan iliweza kuteka eneo la Jabal Kala al-Laban, lililo karibu na mpaka unaozozaniwa, kufuatia shambulio la anga, kwa mujibu wa afisa wa  kijeshi wa Sudan ambaye hakutajwa jina akizungumza na shirika la habari la Reuters.

Siku ya Jumatatu, Ethiopia ilikanusha shutuma za Sudan kwamba jeshi lake lilikamata na kuwanyonga wanajeshi saba wa Sudan na raia mmoja, badala yake ikasema mauaji hayo yametekelezwa na wanamgambo wa eneo hilo.

Duru za serikali ya Sudan zilisema kuwa Sudan imewasilisha malalamiko rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji hayo.

Jeshi la Sudan lilifyatua mizinga ya masafa marefu kuanzia Jumatatu asubuhi hadi Jumanne alasiri, lakini hakuna aliyejeruhiwa, alisema Assefa Ashege, afisa mkuu wa usalama katika eneo la Amhara nchini Ethiopia.

Wakaazi wawili wa eneo hilo walisema kuwa jeshi la Sudan limechukua udhibiti wa eneo la Jabal Kala al-Laban.

Mzozo kuhusu al-Fashaqa, ambayo ipo ndani ya mipaka ya kimataifa ya Sudan lakini imekaliwa na wakulima wa Ethiopia kwa miongo kadhaa, umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni sambamba na mzozo wa kidiplomasia kuhusu ujenzi wa Ethiopia wa bwawa la kufua umeme wa maji.