Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili akiongea na waandishi habari (hawapo pichani) kuhusu dhamira ya Benki hiyo kuendelea kutoa elimu ya fedha kupitia promosheni ya Mzigo Flexi ambapo Benki ya CRDB inalenga kuwafikia Watanzania katika vitongoji vyote vya Jiji laDar es salaam na Tanzania kwa ujumla ili kutoa elimu ya mpango maalum wa kuweka akiba ambao utawawezesha kupata riba ya hadi asilimia 9. Kulia ni Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Benki ya CRDB, Badru Idd na Meneja wa Tawi la Azikiwe, Hamis Saleh.
===== ===== =====
Benki ya CRDB imejipanga kuendelea kutoa elimu ya fedha kupitia promosheni ya Mzigo Flexi ambapo inalenga kuwafikia Watanzania katika vitongoji vyote vya Jiji la Daes salaam na Tanzania kwa ujumla, lengo likiwa kutoa Elimu ya mpango maalum wa kuweka akiba ambao utawawezesha kupata riba ya hadi asilimia 9.
 
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika katika viunga vya Tawi la CRDB Benki lililopo Mtaa wa Azikiwe jijini Dar es salam Mapema leo, Mkuu wa kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili alisema; “Sisi kama Benki tumeamua kuwafikia Watanzania na kuwapa elimu ya fedha ili kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba kwa malengo ya muda mfupi, kati na mrefu”.
 
"Sambamba na kuwapa elimu lakini pia kupitia mpango huu Benki inatoa riba ya hadi asilimia 9 ili kutoa hamasa ya kuweka akiba ambapo kupitia promosheni ya Mzigo Flexi, mteja anaweza kuweka amana kwa muda wa kati ya miezi 3, 6, 12 au 24,” alisema Adili.
Promosheni ya ‘Mzigo Flexi’ inalenga watu binafsi, vikundi, taasisi na wafanyabiashara na mteja anaweza kuwa na mpango wa akiba wa ‘Mzigo Flexi’ zaidi ya mmoja na kuwekeza kwenye mikataba mingi. Kila mkataba utakuwa ni mkataba huru na bidhaa haina ada yoyote na riba inalipwa kwa akaunti ya kibinafsi ya mteja kulingana na kipindi cha riba kilichokubaliwa (Kila mwezi, Robo mwaka, Nusu mwaka, Kila mwaka au wakati wa kukomaa).
 
Iwapo mteja ataamua kughairi utaratibu wa ‘Mzigo Flexi’, atalazimika kupoteza asilimia 50 ya riba aliyopata na kuendelea kuweka fedha chini ya utaratibu mwingine wa kawaida wa benki.
Wateja wanaweza kupata mpango wa akiba wa “Mzigo Flexi” huo kupitia tawi lolote la Benki ya CRDB nchi nzima lakini pia anaweza kupata fomu ya maombi kupitia tovuti ya Benki na kuwasilisha katika tawi lolote la Benki ya CRDB baada ya kuzijaza.