Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ya shilingi trilioni 14.94.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kugharamia matumuzi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka huo wa fedha wa 2022/2023.

Akiwasilisha bajeti ya wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kati ya fedha hizo shilingi trilioni 13.6 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na trilioni 1.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Kuhusu usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma Dkt. Nchemba ameliambia Bunge kuwa watafanya mapitio na ujenzi wa mfumo mpya wa usimamizi wa ununuzi wa umma na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya ununuzi katika taasisi nunuzi.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma – PPRA inatarajia kuanza ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu jijini Dodoma na ofisi ya kanda jijini Dar es Salaam, kuwezesha mafunzo kwa watumishi 940 kutoka katika Taasisi Nunuzi 170 na wazabuni 1,200 ambao wamejisajili katika mfumo wa TANePS, kufanya mapitio na ujenzi wa mfumo mpya wa usimamizi wa ununuzi wa umma na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya ununuzi katika Taasisi Nunuzi 530” amesema Dkt. Nchemba

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, wizara ya Fedha inakadiria kukusanya maduhuli ya jumla ya shilingi trilioni 1.05 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na gawio, kodi za pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na mauzo ya leseni za udalali.