Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali hapa nchini kuhusu fursa zitokananzo na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ili kuwawezesha kuzichangamkia kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa  tarehe 29 Mei 2022 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati akifungua rasmi Warsha ya Kueleimisha na Kujenga Uwezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Mkataba ulioanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mhe. Balozi Mbarouk amesema kuwa, watanzania wana kila sababu ya kuchangamkia fursa zinazotokana na Mkataba wa AfCFTA na kunufaika nazo kwa kuwa Tanzania ni mwanachama kamili wa mkataba huo baada ya Bunge kuuridhia mnamo mwezi Januari 2022. Fursa hizo ambazo ni pamoja na Biashara, Ajira, Uwekezaji, Teknolojia zitainufaisha nchi kwa kukuza pato la Taifa kutokana na eneo kubwa la soko, kukuza viwanda, ongezeko la biashara ndani ya Afrika na kuongezeka uzalishaji na mnyororo wa thamani.

“Ili kuwawezesha wadau kutambua na kutumia fursa za AfCFTA, Serikali imejipanga kuwa na mkakati endelevu wa kutoa elimu kwa umma. Tayari Serikali imeanza kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wadau kwa makundi. Tayari Warsha za aina hii zimefanyika Zanzibar, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza na zimehusisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi” amesema Mhe. Mbarouk.

Ameongeza kusema kuwa, AfCFTA ni muhimu kwa Tanzania katika kupanua wigo wa soko la bidhaa na huduma nje ya soko la EAC na SADC na kwamba Wizara inatumia fursa ya AfCFTA kutekeleza mikakati ya Diplomasia ya Uchumi ya kuvutia wawekezaji  nchini ilikuzalisha na kuuza kwenye soko la AfCFTA.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Mabalozi kwenye suala hilo na kushirikiana na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wadau ili Tanzania itumie ipasavyo fursa zitokanazo na ushiriki wake katika AfCFTA.

“Nina imani kuwa kupitia warsha hii, kila mmoja wetu atakuwa amepata elimu ya kutosha kuhusu mkataba wa AfCTA pamoja na fursa zake na mtakuwa mabalozi wazuri kwenye suala hili katika kushirikiana na Serikali” alisisitiza Balozi Mbarouk.

Akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa AfCFTA, Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule amesema nchi  54 za Afrika zimesaini Mkataba huo na tayari nchi 43 ikiwemo Tanzania zimeuridhia.  Amesema malengo ya kuanzishwa mkataba huo ni pamoja na kutengeneza soko moja la uhakika la kuhimili vishindo vya dunia; kujenga na kukuza uzalishaji na uwezo wa uchumi wa viwanda barani Afrika  na kuweka msingi utakaowezesha kuwa na umoja wa forodha wa Afrika.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe.Vincent Mbogo ameipongeza na kuishukuru Wizara kwa kundelea kutoa elimu na kushauri jitihada zaidi zitumike ili kuwafikia wananchi wa mijini na vijijini. Pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwa na takwimu sahihi za mahitaji ya soko na zile za uzalishaji ili kuwe na uwiano na mwendelezo kwenye ufanyaji biashara. Vilevile elimu ya uzalishaji wa bidhaa bora na zenye viwango itolewe ili kukidhi matakwa ya Soko hilo.

“Naipongeza Wizara kwa hatua hii. Hata hivyo bado mna kazi kubwa ya kuwafikia watu wa mijini na vijijini ili kuwaeleimisha kuhusu fursa zitokanazo na soko hili muhimu. Tumieni njia mbalimbali kutoa elimu hii ikiwemo vyombo vya habari kama radio, televisheni na mitandao ya kijamii ili elimu hii iwafikie wananchi kwa wingi” alisema Mhe. Mbogo.