Waziri Mulamula Afanya Mazungumzo Na Naibu Wa Usalama Wa Taifa Wa India
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa India Mhe. Vikram Misri jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao yalijikita kujalidi masuala mbalimbali kuhusu ulinzi na usalama katika ngazi ya Kitaifa, Kanda na Kimataifa kama vile changamato za wahamiaji haramu, ushafirishaji haramu wa binadamu, ugaidi na uharamia.
Waziri Mulamula amemweleza Mhe. Misri kuwa hali ya usalama ndani ya nchi na kwenye mipaka ya nchi yetu ni salama na tumekuwa tukiendelea kushirikiana vizuri na nchi jirani zinazotuzunguka na Jumuiya za kikanda katika kutatua changamoto mbalimbali kama vile usafirishaji haramu wa binadamu, uharamia na masuala ya ugaidi.
Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa India Mheshimiwa Balozi Vikram kwa upande wake ameeleza kuridhishwa kwake na namna Serikali ya Tanzania inavyoshiriki kutatua na kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama katika ngazi ya Taifa, Kikanda na Kimataifa. Vilevile aliongeza kusema kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Tanzania katika eneo la ulinzi na usalama.
Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa India H.E Amb. Vikram Misri yupo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo anatarajia kuonana na viongozi mbalimbali wa Serikali.