WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi miwili kwa watumishi 30 wa Halmashauri ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Magesa Mafuru wawe wame merejesha fedha za umma walizozitumia kinyume na utaratibu.

 Mheshimiwa Majaliwa amemkabidhi Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza, Bw. Mashauri Elisante majina ya watumishi hao kwa hatua zaidi. “Kama kuna mtumishi wa umma anayedhani kwamba awamu hii ni ya mchezo anajidanganya Serikali itashughulika nae. Wakuu wa Mikoa na wilaya wachukue hatua ili kujenga nidhamu kwa watumishi.”

 “Taarifa ya uchunguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa fedha za miradi ya maendeleo imethibitisha kwamba  baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Sengerema hawaendi sambamba na matarajio ya Serikali ya awamu ya sita suala ambalo halikubaliki.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Mei 7, 2022) wakati akizungumza na Madiwani na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Sengerema katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Sengerema akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo zinazotekelezwa mkoani Mwanza. Amemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo ahakikishe watu wote waliotajwa wanarejesha fedha hizo kwa wakati.

Mheshimiwa Majaliwa amewataja watumishi wanaotuhumiwa katika ubadhirifu huo kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mweka Hazina kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato, Watendaji wa Kata tisa na Watendaji wa Vijiji watatu, Maafisa Uvuvi sita, Afisa Mifugo mmoja, Mawakala wa Makusanyanyo wanane na Afisa Mapato mmoja.

Amesema taarifa hiyo ya CAG imeonesha uwepo wa tuhuma kuhusu udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri hiyo. “Serikali haiwezi kuwavumilia na itachukua hatua kali kwa wote waliohusika na ubadhilifu huo.”

Amesema uchunguzi huo ulifanyika baada ya CAG kupokea tuhuma kuhusu udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza. Taarifa hiyo aliipokea Januari 10, 2021.

Waziri Mkuu amesema baada ya uchunguzi huo CAG alibaini kwamba halmashauri hiyo ilikusanya shilingi bilioni 3, 027,518,982 katika mfumo wa kukusanyia mapato (LGRCIS) pamoja na namba za utambulisho 87.

“Hata hivyo kiasi cha shilingi milioni 645,245,926 ya makusanyo hayo haikuwasilishwa benki na wakusanyaji kinyume na utaratibu. Pia shilingi milioni 115,158,750 kilioneshwa kwenye mfumo wa kukusanya mapato kama makusanyo ya fedha taslimu wakati ilikuwa ni miamala iliyokosewa.”

Waziri Mkuu amesema kuwa kiasi kingine cha shilingi milioni 79,578,395 zilitumika kugharamia shughuli za halmashauri ambazo hazikuainishwa na shilingi milioni 280,234,248 zililipwa kwa mawakala wa ukusanyaji kama kamisheni kwa idhini ya Mkurugenzi Mtendaji wa wakati huo bila ya fedha hizo kuingizwa kwanza benki kama sheria inavyoelekeza.

Amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 7,226,800 hakikukusanywa kufuatia leseni mbili za biashara namba 17 na namba 71 kutolewa kwa bei pungufu na kutolipwa gharama za leseni. Hata hivyo kiasi cha shilingi milioni 227,735,099 za leseni ya huduma hakikukusanywa kutoka kwa makampuni na taasisi mbalimbali na halmashauri.

“Kiasi cha shilingi milioni 652,989,548 kiliekezwa kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 na 2019/2020 kutoka katika makusanyo ya ndani ya halmashauri licha ya kuwa kwenye bajeti hazikukupelekwa kwenye miradi husika.

 “Halmashauri haikukusanya jumla ya Shilingi 141,838,305.24 kutoka katika mradi wa upimaji wa viwanja eneo la Nyakato, Isamilo, Kilabela, Nyamatongo na Busisi katika mwaka wa fedha 2018/2019 na kusababisha kutorejesha kiasi cha shilingi milioni 65.2 kilichoazimwa kutoka Wizara ta Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajiri ya mradi huo.”

Kufuatia ubadhilifu huo, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kote wafuatilie taarifa za fedha zote zilizopelekwa kwenye miradi katika Halmashauri zao na waimarishe usimamizi kwa kuzingatia thamani ya fedha na muda wa utekelezaji.

“Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote kuwasilisha kwa Kamati za Siasa za Mikoa na Wilaya Taarifa za Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita ifikapo tarehe 20 Mei, 2022.  Lengo ni kuwawezesha Viongozi wa Chama katika ngazi husika kuifahamu, kuikagua na kuitolea taarifa kwa Wananchi.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesisitiza  kuwa watumishi wa umma  wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, nidhamu, maarifa na ubunifu.   “Nawasihi nyote muache kufanya kazi kwa mazoea, mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji mbalimbali wajenge utaratibu wa kusikiliza hotuba mbalimbali za viongozi wakuu wa nchi na kuyafanyia kazi maelekezo yanayohusu maeneo yao.