NA Angela Msimbira – Musoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Palela Nitu Msongela kujitathimini utendaji wake kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Hospital ya Wilaya na Ujenzi wa jengo la Halmashauri.

Kauli hiyo ameitoa  Mei 7 Mei, 2022 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Halmashauri na Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoani Mara.

Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe kuunda timu ya uchaguzi ili kujiridhisha iwapo thamani ya fedha umezingatia katika ujenzi wa Miradi ya Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Hospitali ya Wilaya inayojengwa katika kijiji cha Suguti, Mkoani Mara.

Waziri Bashungwa amesema miradi mingi ya Halmashauri hiyo imekuwa ikidorora na kujengwa kwa kusuasua na kupelekea miradi mingi kutokukamilika kwa wakati.

“Ninamuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha a aunda timu ambayo itachunguza matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa miradi hiyo ili kuona dhamani ya fedha iliyotumika inaenda sambamba na ubora wa majengo yaliyojengwa“ amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi kusimamia ujenzi wa miradi hiyo na kumtaka kutumia Kamati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya Mkopo wa IMF kusimamia ujuzi wa Miradi hiyo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe Ally Hapi amesema kuwa wataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo na watumishi watakaobainika ni wabadhilifu katika miradi watachuliwa hatua za kiutumishi.