Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri pamoja na viongozi wengine kuzima magari yao wanapokuwa hawayatumii/hawamo ndani ya magari ili kuunga serikali mkoano katika jitihada za kubana matumizi.

Amesema hayo bungeni jijini Dodoma akieleza kwamba kumekuwepo na utaratibu usio sahihi wa baadhi ya magari ya viongozi wanapokuwa bungeni wanayaacha yanaunguruma kwa muda wote wa vikao, jambo ambalo linaiongezea serikali mzigo wa gharama za mafuta.

“Tunatamani tuone magari ya kiongozi, yakishamshusha kiongozi, sio tu hapa bungeni, nchi nzima, awe ni mwenyekiti wa halmashauri, awe ni meya, awe ni katibu mkuu, ukiacha viongozi ambao kwa itifaki magari yao inabidi yaendelee kuwaka, magari mengine yakishamshusha kiongozi yazimwe na dereva ashuke,” amesema Dkt. Tulia.

Ameeleza kuwa gharama za mafuta zinaendelea kuwa kubwa kwa sababu ya kuacha magari yakiwaka hata yasipotumika wakati mwingine hadi kwa saa.

“Tunatamani tuone mabadiliko kwenye hilo eneo,” amesema Dkt. Tulia akieleza kwamba mtu anapokuwa anaendesha gari lake akiwa kwenye foleni anazima, sasa kwanini gari la serikali aliache linaunguruma wakati halitumiki.