Na. James K. Mwanamyoto-Bahi
Urasimishaji wa ardhi, utoaji wa hatimiliki za kimila na ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi za masijala unaofanywa kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) katika vijiji vya Msisi na Makanda wilayani Bahi utasaidia kutatua migogoro ya ardhi na kutoa fursa za ajira katika vijiji hivyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kutoa hatimiliki na kuweka mawe ya msingi kwenye ofisi za vijiji vya Msisi na Makanda zilizojengwa na MKURABITA katika vijiji hivyo.

Mhe. Jenista amesema, ujenzi wa masijala na urasimishaji uliofanywa wilayani Bahi utawezesha utunzaji mzuri wa kumbukumbu utakaosaidia kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na baina ya mtu na mtu na kuongeza kuwa, Serikali inataka urasimishaji huo uondoe kabisa migogoro ya ardhi.

Sanjali na hilo, Waziri Jenista ameeleza kuwa, urasimishaji ardhi na utoaji wa hatimiliki za kimila kwa wananchi wa vijiji vya Msisi na Makanda umeongeza wigo wa ajira kwa vijana, akina mama na hata wazee kwani hatimiliki walizopatiwa zinawapa fursa ya kukopa kwenye taasisi za kifedha ili kuendesha shughuli za kilimo na ujasiriamali walizopanga kuzifanya.

“Wananchi watakaotumia hati hizo kukopa ili kupata mitaji watalazimika kupata nguvu kazi, na uhitaji huo wa nguvu kazi utatoa fursa za ajira, kama ni shamba litahitaji nguvu kazi na hata kama mkopaji atabuni mradi mwingine tofauti na kilimo atahitaji pia nguvu kazi hivyo ataajiri tu,” Mhe. Jenista amefafanua.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato Serikalini, Mhe. Jenista amesema kuwa urasimishaji ardhi una faida kubwa katika kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na sio kwenye halmashauri tu kwani mwisho wa siku yanaongeza pato la taifa.

Aidha, Mhe. Jenista amesema kuwa urasimishaji wa ardhi uliofanyika umewezesha utoaji wa hati kwa wanawake na wanaume, hivyo kuondoa dhana potofu ya unyanyasaji wa wanawake katika suala la umiliki wa ardhi kwenye vijiji vya Msisi na Makanda wilayani Bahi.

“Utoaji wa hati hizi kwa wanawake na wanaume unadhihirisha kuwa kwenye suala la umiliki wa ardhi wote wana haki sawa, hivyo umeondoa mila ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye umiliki wa ardhi,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kwa upande wake, Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema ofisi yake imetumia muda mfupi sana kupima mashamba 1483 kwenye Kijiji cha Msisi wilayani Bahi na kuongeza kuwa upimaji huo uwemewezekana kwasababu wananchi wa kijiji hicho wametoa ushiririkiano wa kutosha.

Dkt. Seraphia amesema, wananchi waliokabidhiwa hati wamepata ufunguo wa kufunga mlango wa umaskini na kufungua mlango wa utajiri iwapo watazitumia hati hizo kuomba mikopo ya kuendesha shughuli za kilimo na ujasiriamali ili kunyanyua maisha yao kiuchumi.

Naye, Mwakilishi wa Meneja wa NMB tawi la Bahi, Bw. Benson Mwande amemthibitishia Waziri Jenista na wananchi wa vijiji vya Msisi na Makanda kuwa hati walizokabidhiwa zinatambuliwa na benki yao na kuongeza kuwa, mpaka sasa wananchi 15 wameomba mikopo na 15 wengine wameomba kufungua akaunti katika benki hiyo tawi la Bahi.

“Siku ya Jumatano tarehe 05 Mei, 2022 NMB tutakuja katika Kijiji cha Msisi kwa ajili ya kutoa huduma za kukopesha na kufungua akauti kwa wananchi waliopatiwa hati za hakimiliki za kimila,” Bw. Mwande amesisitiza.

Utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) unaofanyika katika maeneo mbalimbali nchini umepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuboresha Maisha ya wananchi wenye kipato cha chini kwa kurasimisha ardhi na biashara zao.