Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi La Polisi Mkoani Mwanza Kuelekea Sikukuuu Ya Eid-el Fitr
Tukio la kwanza
Kuelekea Sikukuu ya Eid –Elfitri
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga vyema katika kuhakikisha sherehe za sikukuu ya Eid –Elfitri zinasheherekewa kwa amani na utulivu, hivyo tuwatoe hofu wananchi kwani ulinzi umeimarishwa.
Aidha katika Nyumba za Ibada-Misikitini ulinzi umeimarishwa vyakutosha kwani Askari watakua wakipita kwa doria za miguu, pikipiki na magari katika maeneo yote ya Jiji na Mkoa wa Mwanza. Pia tuwatake Wananchi wanapokwenda kwenye Nyumba za ibada au kumbi za starehe wasiache nyumba zao bila uangalizi au kiziacha wazi kwani kunaweza kushawishi wezi kuiba.
Pia tuwakumbushe wazazi na walezi kuwa pamoja na kusherekea sikukuu hii wasisahau majukumu yao ya kuwa makini na watoto wao kwa kutowaacha peke yao barabarani na katika sehemu za michezo mfano maeneo ya beach/mialo na kwenye bembea, hata hivyo disco toto ni marufuku. Vilevile ni marufuku kwa madereva wa vyombo vya moto kuendesha wakiwa wamelewa au mwendo kasi, endapo ikibainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawatakia wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla sikukuu njema ya Eid Elfitri. Lakini pia kusheherekea Sikukuu hii kwa amani na utulivu.
Tukio la Pili.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakata watuhumiwa 21 kwa kosa la kuvunja ghala usiku na kuiba Televisheni 167 mali ya kampuni ya ZAK- Solution –Kampuni ya wachina inayojihusisha na uingizaji wa Televisheni Nchini.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha wiki mbili za mwishoni mwa mwezi wa nne katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza na Mikoa jirani ya Shinyanga na Simiyu limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 21, wa kosa la kuvunja ghala usiku na kuiba Televisheni 167, zenye ukubwa wa Inchi 43 aina ya SAMSUNG mali ya kampuni ya ZAK-Solution, zenye thamani ya Tsh 329,000,000/=, kitendo ambacho ni kinyume na sheria
Tukio hilo lilitokea tarehe 30.03.2022 majira ya 21:00hrs huko maeneo ya Kapripoint kwenye jengo la NSSF lililopo wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza, hii ni baada ya wahalifu hao kushirikiana na walinzi ambao walikua wanalinda jengo hilo kuvunja na kuiba televisheni hizo, ndipo ufuatiliaji ulianza mara moja na kufuatia taarifa za kiintelejensia Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa tajwa hapo juu pamoja na televisheni 115. Msako mkali bado unaendelea kufanyika katika maeneo yote ili kuwakamata watuhumiwa ambao bado hawajapatikana pamoja na televisheni ambazo hazijapatikana. Upelelezi wa shauri hili bado unaendelea.
Tukio la tatu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia Watu watano kwa tuhuma za Mauaji ya Mwalimu wa shule ya wasichana ya Bwiru.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya Mwalimu Ambrose Mapembegashi, miaka 59, wa Shule ya Sekondari ya Wasicha ya Bwiru, aliyefariki baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani kisogoni. Wahalifu baada ya kutekeleza mauaji hayo walichukua TV aina ya ITEL Model A243LAE, Subwoofer aina ya Sapiano model no SP 661 na Pasi aina ya Africab model JT-22512, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Tukio hilo limetokea tarehe 29.04.2022 majira ya 22:00hrs huko maeneo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwiru katika makazi ya walimu, kata ya Pasiansi, Wilaya ya Ilemela, hii ni baada ya wahalifu kuingia kwenye nyumba ya marehemu na kutekeleza mauaji hayo na kuchukua mali tajwa
hapo juu. Jeshi la Polisi lilipata taarifa juu ya tukio hilo ndipo ufuatiliaji wa haraka ulifanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu hao pamoja na mali walizoiiba maeneo ya nyasaka, kitangiri na bwiru.
Watuhumiwa waliokamatwa ni;-
Justine Lucas, miaka 33.
Daniel Edward, miaka 27, Mkazi wa Bwiru.
Pascal Nyamhanga, miaka 22, Mkazi wa Kitangiri.
Hussein Swalehe @Kisesa, miaka 23, Mkazi wa Jiwe kuu na
Elisha Jonas, miaka 25, mkazi wa Bwiru Press.
Upelelezi wa shauri hili unakamilishwa na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara moja.
Tukio la nne
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia wahamiaji haramu 68, raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia Nchini bila kibali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji tarehe 29.04.2022 majira ya 17:30hrs katika kijiji cha Sanjo, kata ya Usagara, Wilaya ya Misungwi, baada ya kupatikana kwa taarifa za kiintelejensia lilifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 68, raia wa Ethiopia wenye umri kati ya miaka 14 hadi 25 ambao wameingia Nchini bila kibali wakisubiri kusafirishwa kwenda Nchini Afrika kusini. Wahamiaji hao walikuwa wamehifadhiwa na mwanamke aitwayeTarica Alex @ Mlawa, miaka 26 ambaye pia amekamatwa, kwenye nyumba ya mtu aliyefahamika kwa jina moja la Joseph. Uchunguzi unakamilishwa kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na mara moja watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa taratibu za kisheria.