WAZIRI wa Nishati, January Makamba leo Jumanne Mei 10, 2922 amesema Serikali imetoa ruzuku ya Tsh bilioni 100 kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini.

Akizungumza Bungeni Waziri Makamba amesema ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka2021/22.

Amesema Kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea

“Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali. Ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini.

“Ruzuku hii ya Sh100 bilioni itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa” amesema Makamba.

Pia waziri Makamba amesema hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na:

Kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo.

Kuanzisha mfuko wa kuhimili ukali wa bei zamafuta (Fuel Price Stabilization Fund).

Kuanzisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve).

Kuwa na kituo kikubwa cha mafuta (PetroleumHub).

Kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghalamoja(Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi.

Kuiongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi.

Kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja).