Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kurekebisha posho ya kujikimu ya safari za ndani ya nchi kwa watumishi wa umma na kiwango cha malipo ya kazi maalum (Extra Duty) kwa watumishi wa umma nchini ambapo utekelezaji wake unaanza rasmi Julai 1, 2022.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kutokana na kibali hicho, posho ya kujikimu ya safari za ndani kwa kiwango cha juu imepanda kutoka shilingi 120,000/= hadi 250,000/= na kiwango cha chini kutoka shilingi 80,000 hadi 100,000/=.

Ameongeza kuwa, kiwango cha malipo ya kazi maalum kimeongezeka kwa ngazi zote, ambapo kwa ngazi ya chini kimepanda kutoka shilingi 15,000/= hadi 30,000/=, kwa ngazi ya kati kimeongezeka kutoka shilingi 20,000/= hadi 40,000/= na kwa ngazi ya juu kimeongezeka kutoka shilingi 30,000 hadi 60,000/=

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, viwango hivyo vipya vitalipwa na Serikali kupitia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, hivyo taasisi zisiombe nyongeza ya bajeti ili kuwalipa viwango hivyo watumishi wake.

Kufuatia ongezeko hilo, Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa Watumishi wa Umma wote nchini kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais za kuboresha maslahi wa Watumishi wa Umma.