SERIKALI imeuelekeza uongozi wa  Kampuni ya  Gas Entec Tanzania ambayo inajenga meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi  Tu kuzingatia makubaliano  yote   yaliyomo kwenye mkataba wa ujenzi wa meli hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa  Kassim Majaliwa  Mei 14, 2022  katika kikao kati yake na Balozi wa Korea ya Kusini nchini, Kim Sun Pyo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam.  

Katika  Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania  Bw. Kwak ambaye alikiri  mapungufu katika utekelezaji wa mradi huo na aliahidi kuwa kampuni yake itaongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa wakati na meli hiyo iwezo kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.

Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza  kuwa  watalaamu wa Kampuni ya  Gas Entec Tanzania warejeshewe Pasi zao za kusafiria ambazo zilizuiwa na s

Serikali  kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mwenendo wa ujenzi wa meli hiyo.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Mbarouk Mbarouk na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Fred Mwakibete.

Wengine ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa  Kampuni ya Huduma za meli, Philemon Bagambilana  na Kanali Samwel Mahirane ambaye ni Kamishina wa Uhamiaji, Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka nchini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU