SERIKALI imetangaza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Elimu hapa nchini  kuanzia Shule ya Msingi hadi Sekondari. Mabadiliko hayo yamelenga kuwaandaa wanafunzi kujifunza kwa vitendo katika masomo ya kilimo, Sayansi kimu (Home Economics), Ufundi na biashara (Book-Keeping na Cormmerce).

Mafunzo hayo ya vitendo  yatawawezesha wanafunzi  kupata ujuzi wa  kukidhi matakwa ya ajira ikiwemo kwenye sekta ya kilimo, Utalii  na biashara.

Kupitia Mpango huo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeweka mipango ya kuwandaa Walimu kwa kuwapa mafunzo  endelevu kazini ili kuwapatia uwezo wa kuwafundisha wanafunzi vizuri.
 
Mkakati huo umetangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (Mb) jana tarehe 4/5/2022 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa walimu 322 wa masomo ya Mchepuo wa kilimo na Sayansi kimu kutoka mikoa ya yote ya Tanzania Bara na Zanzibar yanayofanyika Mkoani Morogoro.

 
Prof.  Mkenda amesema tayari Wizara hiyo imeanza kutoa kipaumbele kwa mafunzo ya walimu wa masomo hayo hapa nchini kwa kuwaongezea ujuzi na maarifa ya kwenda kuwafundisha wanafunzi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
 

“Tunataka kuwandaa vijana ambao wataweza kuongeza ajira katika sekta ya kilimo, Biashara  na utalii ambao tayari umeshatangazwa nje ya nchi na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya Utalii ya “ The RoyarTour.
 
Kwa Upande wake, Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt.  Aneth Komba, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kitalaamu walimu wa masomo ya Sayansi kimu na Kilimo kwa kuwapa mbinu za ufundishaji, ujifunzaji na upimaji unaozingatia ujenzi wa umahiri.
 
Dkt. Komba alisema kuwa matokeo ya mafunzo hayo yatamuwezesha muhitimu wa masomo hayo kupata maarifa, stadi za kutenda na uelekeo wa kujitegemea kwa manufaa mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.

 
‘Mafunzo haya yanawajengea walimu hawa uwezo mkubwa  ambao watakwenda kuuambukiza kwa walimu wengine na baadae kwa walimu wanaowafundisha  ambao wataingia katika soko la ajira na wengine kuweza kujiajiri” amesema Dkt. Komba.
 

Kwa upande wa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Hadija Mcheka, amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati kutokana na kuwepo kwa upungufu mkubwa wa walimu wa masomo hayo na kwamba wataendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusaidia kuongeza idadi ya walimu wanafundisha masomo hayo hapa nchini.