Imeelezwa kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa mazao yote nchini kwa msimu wa kilimo wa Mwaka 2022/ 2023.

Hayo yamebainishwa  tarehe 17 Mei, 2022 na Waziri wa kilimo Husen Bashe alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika kikao cha bunge cha 13 kinachoendelea jijini Dodoma.   

Waziri Bashe ameziagiza  kampuni na viwanda vyote vya mbolea nchini kusajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ifikapo tarehe 31 Mei, 2022 ili kurahisisha utoaji na usimamizi wa ruzuku.

Akielezea namna ya utoaji wa ruzuku hizo Waziri Bashe alisema mifuko ya mbolea itawekwa barcode nalabel ya ruzuku ili kutofautisha na mbolea zitakazoendelea kuuzwa sokoni bila ruzuku.

Pamoja na hayo, Waziri Bashe amesema kampuni yeyote ambayo haitatekeleza agizo hilo na kukubali kutumia mfumo utakaowekwa na TFRA wa kusimamia na kusajili kampuni na mawakala kwa kuweka eneo la biashara kwenye maduka na ghala zao mikoani serikalihaitosita kuwafutia leseni zao za biashara.

Aidha, Waziri Bashe amebainisha kuwa mfumo huo wa mbolea ya ruzuku utawapa kipaumbele wazalishaji wa ndani ili kulinda viwanda vya ndani, ajira na usalama wa chakula.

Amesema, Wizara itaendelea kuwalinda na kuwawezesha wawekezaji wa viwanda vya ndani ikiwepo intracom fertilizer Limited chenye uwezo wa kuzaisha tani 600,000 (laki sita) mbolea pamoja na kushirikiana na kuwezesha upatikanaji wa vivutio vya uwekezaji kwa kiwanda cha mbolea Minjingu ili kuongeza uwezo wake wa kuzalisha kutoka tani 100,000 za sasa.

Vilevile Waziri Bashe amewahakikishia wazalishaji wadogo wa mbolea hai organic na chokaa kuwa itaendelea kuwalea, kuwalinda, na kuwahakikishia masoko ili kupunguza gharama za kuagiza aina hiyo ya mbolea kutoka nje ya nchi na kuwataka wazalishaji wadogo wa aina hiyo ya mbolea kufika wizarani ili kuweza kusaidiwa.

Akizungumzia manufaa ya ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mahusiano na nchi za Afrika Mashariki,  waziri Bashe amesema ni pamoja na kumpata mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha mbolea cha Intracom Fertilizer Limited kinachojengwa Jijini Dodoma na mwekezaji kutoka nchini Burundi.

Amesema uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho unagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 180 huku kikitarajiwa kuzalisha kiasi cha tani laki sita (600000) za mbolea kwa mwaka na kutoa ajira za kudumu kwa watanzania 3000.

Ameendelea kusema, wizara imeendelea kuratibu uzalishaji na uingizaji wa mbolea nchini ambapo tani 436,452 za mbolea zimepatikana kwa msimu wa kilimo wa 2021/2022  ikiwa ni asilimia 63 (63%) ya mahitaji yote ya mbolea na kubainisha kuwa tani 274000 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 43000 zimezalishwa katika viwanda vya ndani wakati kiasi cha tani 117 900 ni bakaa ya msimu uliopita wa kilimo.