Uturuki imesema itapinga mpango wa Sweden na Finland wa kutaka kujiunga kwenye mfungamano wa kijeshi wa NATO. 

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema  kwamba amewaambia washirika wa NATO kwamba Uturuki inapinga hatua ya kujiunga kwa nchi hizo mbili. 

Erdogan amesema pingamizi la Uturuki linatokana na matatizo yaliyopo kati ya nchi yake na Sweden na Finland ambapo Uturuki inazilaumu nchi hizo kwa kuwapa hifadhi wafuasi wa Fethullah Gulen, kiongozi wa dini ya Kiislamu mwenye makazi yake nchini Marekani ambaye Uturuki inamlaumu kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwaka 2016. 

Uturuki imesema inazitaka Finland na Sweden ziache kuwapa misaada Wakurdi wanaoipinga Uturuki na pia ziondoe vikwazo vya silaha walivyoweka dhidi ya nchi hiyo.