Rais Samia Awahakikishia Wafanyakazi Nyongeza ya Mishahara Ipo
Rais Samia Suluhu Hassan amewahikikishia wafanyakazi nchini kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 itaongeza mishahara kwa watumishi wake.
Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Mei Mosi 2022 wakati wa sherehe za wafanyakazi duniani zinazofanyika katika uwanja wa Jamuhuri jijini hapa.
Hata hivyo, alisema nyongeza ya mishahara haitakuwa na kiwango ambacho kimependezwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) la Sh1.01 milioni kwa mwezi kwa sababu ya hali ya uchumi wa Taifa na dunia sio nzuri.
“Uchumi wetu ulishuka chini sana, tumejitahidi sana kwasababu nilishatoa ahadi mwaka jana (ya kupandisha mishahara), nimeagiza liwepo, mahesabu yanaendelea tutajua lipo kwa kiasi gani lakini jambo lipo,” amesema.
Kuhusu wafanyakazi waliofukuzwa kazi kwa vyeti feki lakini walifanya kazi kwa muda mrefu, Rais Samia amesema ameagiza Wizara ya Fedha wakae na wizara (Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) kuangalia ni kiasi gani walikatwa kwenye jasho la mishahara yao na kuchangia katika mifuko ya jamii ili waweze kulipwa jasho lao.
“Waangalie walitoa kiasi gani lakini nasisitiza kile asilimia tano (walichochangia kutoka katika mishahara yao) na kuacha ile ya asilimia 10 ya mwajiri,” amesema.
Pia amesema ameziagiza wizara hizo mbili kuangalia kiasi gani kitagharimu kuwalipa wafanyakazi waliofanya kazi kwa muda mrefu lakini wakabakisha mwaka mmoja ama miwili kustaafu.
“Na wenyewe waangalie ni kiasi gani kitatugharamu kama tutawapa mafao yao baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu. Tunayafanyia maamuzi baada ya kuona ni gharama kiasi gani Serikali itaingia,”amesema.
Kuhusu kiwango cha kikotoo, Rais Samia amesema kimekuwa na mvutano lakini Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta) limetaka wakutane katikati ya 25 na 50.
“Sasa Serikali itakwenda kukaa katika utatu wetu ama sisi na Tucta kuangalia jinsi tutakavyoenda kufanya. Lakini wazo mliokuja nalo sio baya. Ombi langu kwenu Tucta mtoe ushirikiano wa kutosha ili kwa mwaka huu ukimalizika lifanikiwe,”amesema.
Rais Samia amesema hakuna mshahara wala mafao yanayotosha lakini angalau kikotoo kiwe kwa kiwango cha kuridhisha.