Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya utatekeleza taratibu mpango wa kupiga marufuku mafuta kutoka Urusi. Hayo ni wakati Umoja huo umezindua msururu wa vikwazo vipya vya kuiadhibu Urusi kwa kuivamia kijeshi Ukraine. 

Von der Leyen ameliambia bunge la Ulaya leo mjini Strasbourg kuwa Ulaya itaondokana na matumizi ya mafuta ghafi ya Urusi katika kipindi cha miezi sita na kisha mafuta yaliyosafishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. 

Pendekezo la von der Leyen limeomba kuwa Hungary na Slovakia ambazo zinategemea pakubwa mafuta ya Urusi, zipewe muda zaidi wa kuanza kutekeleza mafuruku hiyo. 

Mabalozi 27 wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana leo kuutathmini mpango huo na utahitaji kuidhinishwa kwa kauli moja ili kuanza kutekelezwa. 

Aidha wanachama wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kukubaliana kuwa benki kubwa kabisa ya Urusi, Sberbank iondolewe kwenye mfumo wa huduma ya miamala ya kifedha ya kimataifa maarufu kama SWIFT. Orodha hiyo ya vikwazo pia inajumuisha televisheni tatu kubwa za Urusi, mkuu wa Kanisa la Orthodox nchini Urusi na viongozi waandamizi wa kijeshi na serikali.