Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM) Flatei Massay ameruka sarakasi bungeni ikiwa ni kuonyesha msisitizo wa hoja yake kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imekuwa ikitoa ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mbulu hadi Haydom bila utekelezaji.

Flatei ameruka sarakasi leo Jumatatu Mei 23, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/2023.

Flatei amesema licha ya kuahidiwa ujenzi wa barabara hiyo tangu katika bajeti ya mwaka jana, Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeonyesha fedha zilizotengwa mwaka jana zimepelekwa kulipa madeni.

Amesema katika kitabu cha bajeti cha mwaka huu imeonyeshwa kuwa barabara hiyo itajengwa katika kiwango cha lami lakini kwa Kilometa 25.

“Kama waliniahidi kuwa barabara itajengwa hilo tangazo linachukua muda gani? Mimi hapa mheshimiwa Spika sio shilingi tu. Mimi wananchi wameniambia shilingi niichukue niende nayo Mbulu Vijijini maana hapa hamna namna tena,” amesema.

Alimhoji Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kama hamtoi nje ya ukumbi wa Bunge basi apige sarakasi.

“Mimi naona wanataka kunitengenezea ajali kuliko kukitengenezea ajali chama changu si bora uruhusu tu niruke hapa ili wastuke sasa nitafanyaje sasa,”amesema.

Amesema licha ya kusema kwenye bajeti mwaka jana ameuliza maswali saba mwaka jana na manne mwaka huu.

“Mheshimiwa spika nisaidie ninafanyaje? Nimezungumza nao sana sasa inatosha na kwasababu sitaki kuruka hapa. Mipango yote nimefuata utaratibu wote nimefuata inatia uchungu mheshiwa Spika,”amesema.

Amesema kuwa amefuata utaratibu wa kibunge na Serikali ambapo walienda wabunge saba ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kudai barabara.

“Mimi ni mtaalam wa sarakasi hakika nawaambia…zaidi ya hapo unafanya nini mwanaume wa watu,”amesema.

Amesema wanafunzi hawajui barabara ya lami ikoje na kwamba wananchi wa jimbo lake wanaomba Mungu akwame labda ataelewa changamoto wanazopitia.

Baadhi ya wabunge walimwambia aruke sarakasi, hali iliyomfanya mbunge huyo kubinuka sarakasi akitumia meza yake.

Hata hivyo, Dk Tulia alimsihi kutofanya hivyo ambapo aliacha kuendelea kuruka sarakasi huku akimweleza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ama zake.