Korea Kaskazini imefyatua leo kombora la masafa marefu kuelekea bahari yake ya mashariki, ikiwa ni siku chache tu baada ya kiongozi wake Kim Jong Un kuapa kuimarisha zana zake za nyuklia kwa kasi kubwa na kutishia kuzitumia dhidi ya mahasimu wake. 

Jaribio hilo la kombora la Korea Kaskazini ambalo ni la 14 mwaka huu limekuja ikiwa ni siku sita kabla ya rais mpya wa kihafidhina wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol kuapishwa kuongoza kwa muhula mmoja wa miaka mitano. 

Mkuu wa Jeshi la Korea Kusini amesema katika taarifa kuwa kombora hilo lilifyatuliwa kutokea jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo na kuruka kuelekea baharini katika pwani ya mashariki. 

Taarifa hiyo imesema majaribio hayo ya mara kwa mara ya makombora ya Korea Kaskazini ni kitendo cha tishio kubwa kinachohujumu amani ya kimataifa na usalama na kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama yanayopinga jaribio lolote la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini.