Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya Operesheni, Misako na Doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio ikiwemo kukamata watuhumiwa 212 wa makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo kupatikana na nyara za serikali, kupatikana na madini bandia, wizi, uvunjaji, unyang’anyi, utapeli, watoto 39 wa mitaani ambao hulala na kuishi katika mazingira hatarishi katika maeneo SIDO, Mwanjelwa na Mafiati Jijini Mbeya. Aidha kwa kipindi cha mwezi April jumla ya kesi 59 zilipata mafanikio mahakamani na jumla ya watuhumiwa 76 walikutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo jela na kulipa faini.

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.

Mnamo tarehe 05.05.2022 majira ya saa 10:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA huko Mto Mwenje, Kijiji cha Lualaje, Kata ya Lualaje, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili 1. JACKSON CHONGOLO [65] na 2. JIMMY EDSON [37] wote wakazi wa Lualaje wakiwa na Jino la Tembo lenye uzito wa kilogramu 13.7 na thamani ya Tshs. 34,875,500/=.

Aidha watuhumiwa walikutwa na nyama ya Tembo iliyokaushwa yenye uzito wa kilogramu 72 na nyama ya Nyati iliyokaushwa yenye uzito wa kilogramu 57 zote zikiwa kwenye mifuko ya Sulphate wakiwa ndani ya Hifadhi ya Ruaha National Park wakiwa wamebeba kwenye Baiskeli.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA linaendelea na msako wa watuhumiwa wengine. Watuhumiwa ni wawindaji haramu, watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri lao kukamilika.

KUPATIKANA NA MADINI BANDIA.

Mnamo tarehe 29.04.2022 majira ya saa 08:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko maeneo ya Mafiati, Kata ya Maanga, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano [05] kwa tuhuma ya kupatikana na madini bandia.

Watuhumiwa waliokamatwa ni:-

    ERICK DAVID [35] Mkazi wa Chunya.
    ELIAS DAUD [27] Mkazi wa Mabatini.
    MICHAEL MINGA [26] Mkazi wa Ilolo.
    MANENO HUSSEIN [35] Mkazi wa Mafiati.
    EMANUEL HALIDI [35] Mkazi wa Mbalizi.

Watuhumiwa kwa pamoja wamekuwa wakiwalaghai watu pindi wanapokutana nao na  kuomba wapelekwe ofisi za madini kwa madai kuwa wao ni wageni. Lakini mtu huyo akiwa katika harakati za kuwapeleka ndipo wanatoa pakti yenye madini bandia ambayo imebandikwa thamani ya madini hayo Tshs.20,000,000/= na kumuonyesha na kumshawishi awape kiasi kadhaa cha fedha ili yeye aendelee na kutafuta wateja kisha wao hutokomea.  

Watuhumiwa wamekamatwa wakiwa na pakti mbili zenye madini bandia ambazo nje zimebandikwa Tshs.20,000,000/= kuonyesha thamani ya madini hayo. Watuhumiwa huchukua makufuli ya shaba [silver] na kuyayeyusha kisha kutoa vipande vidogo vidogo ambavyo huviweka kwenye pakti ndogo na kuwaaminisha watu kuwa ni madini. Mbali na tukio hilo, watuhumiwa wamekiri kuhusika na matukio kama hayo Mikoa ya Songwe – Tunduma, Rukwa – Sumbawanga na Morogoro.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tunatoa rai kwa wananchi kuacha kununua wala kuuza madini nje ya masko yaliyoidhinishwa na Serikali.

WATAPELI WATU KWA KUJIFANYA WACHUNGAJI.

Mnamo tarehe 08.05.2022 majira ya saa 01:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako maeneo ya Mafiati, Kata ya Maanga, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili 1. SADICK CHONGOLO [43] Mkazi wa Isanga na 2. IVAN WILLIAM [30] Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kujifanya wachungaji.

Ni kwamba awali mnamo tarehe 04.05.2022 watuhumiwa walimtapeli fedha taslimu shilingi 553,500/= Bi.HURUMA KAPESA [30] Mkazi wa Ilolo Jijini Mbeya baada ya kujifanya wachungaji na kumuaminisha mhanga kuwa kiasi cha fedha atakachotoa baada ya kumuombea kitaongezeka zaidi ya kile alichotoa.

Watuhumiwa baada ya tukio hilo la tarehe 04.05.2022 waliendelea na utapeli ambapo mnamo tarehe 08.05.2022 majira ya saa 01:00 Asubuhi wakiwa katika harakati za kuwatapeli watu wengine maeneo ya Mafiati ndipo mhanga Bi.HURUMA KAPESA [30] aliwaona na kutoa taarifa Polisi na kufika eneo la tukio na kuwatia mbaroni watuhumiwa.

Mbali na kumtapeli fedha taslimu shilingi 553,500/= watuhumiwa hao walimtapeli simu mbili aina ya TECNO CAMON yenye thamani ya Tshs.300,000/= na simu ndogo aina ya ITEL yenye thamani ya Tshs.35,000/=, Kikoi, Cheni, Saa na heleni.

Watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kufanya matukio kama hayo mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na visiwani ambapo mkoani Pwani waliwahi kutapeli Tshs.Milioni 18. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, tunatoa rai kwa watanzania wote tusidanganywe na yeyote kwamba anao uwezo wa kukuongezea fedha, fanya kazi kwa bidi kipato utakiona na si vinginevyo.

MTANDAO WA UNYANG’ANYI, UVUNJAJI NA UPORAJI WATIWA MBARONI MBEYA.

Kuanzia tarehe 08.05.2022 hadi tarehe 11.05.2022 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya operesheni na misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya unyang’anyi, uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba na uporaji.

Katika operesheni hiyo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 07 wa matukio ya unyang’anyi, uvunjaji na uporaji ambao ni:-

    AGAY CHRISTOPHER MWISIBILEGE @ UKOPE [28] Mkazi wa Iyela.
    ABDUL ATHUMAN @ RAS [25] Mkazi wa Jacaranda Jijini Mbeya.

Watuhumiwa wamekiri kuhusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha mnamo tarehe 04.04.2022 majira ya saa 08:00 usiku huko maeneo ya Esso, Kata ya Iyela, Jijini Mbeya ambapo walivamia nyumbani kwa KHAMAD KABIBU na kumjeruhi kwa panga sehemu za mkono na kisha kuiba TV Flat Screen mbili aina ya Samsung inchi 32 zenye thamani ya Tshs.2,400,000/=.

Watuhumiwa wengine ni:-

    NUSURA WILSON [18] Dereva Bodaboda, Mkazi wa Ilemi.
    RAZOLO HACHINGA [34] Mkazi wa Makunguru.
    COSTANTINO EDWIN [17] Mkazi wa Makunguru.
    KELVIN LEONARD [26] Mkazi wa Lyoto.
    IPYANA ANANGISYE @ JOTI [25] Dereva Bodaboda, Mkazi wa Masewe – Ilemi.

Katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria katika chumba cha mtuhumiwa IPYANA ANANGISYE @ JOTI [25] alikutwa na mali za wizi na vifaa vya kuvunjia ambao ni:-

    Nyavu ya kuopolea simu.
    Chuma cha kuvunjia Nondo Flat Bar
    Bisibisi.

 Mali za wizi ambazo ni:-

    Makava 50 ya simu.
    Rimoti za TV 11.
    Stendi 13 za TV.
    TV Flat Screen aina ya LG inchi 32.

Aidha watuhumiwa wamekiri kufanya matukio ya unyang’anyi, uvunjaji na uporaji maeneo ya MUST, Mwambene, Airport ya Zamani, Forest Mpya, Isyesye na Esso Jijini Mbeya. Pia wamefanya matukio kama hayo mikoa ya Dar es Salaam na Iringa. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.

KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU.

Mnamo tarehe 04.05.2022 majira ya saa 05:05 asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya misako huko maeneo ya VETA Jijini Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye EDES OISSO [52] Mkazi wa Mushono Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa tuhuma za kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni nne.

Ni kwamba mnamo tarehe 24.04.2022 huko maeneo ya VETA Jijini Mbeya mtuhumiwa EDES OISSO [52] alimtapeli fedha taslimu Tshs. 4,000,000/= JOYCE ATHUMAN [32] Mfanyabiashara na Mkazi wa Ilomba Njia Panda Jijini Mbeya kwa kumlaghai kuwa yeye ana uwezo wa kuzalisha pesa hivyo akimpatia shilingi milioni nne atapata milioni kumi na mbili. Mhanga alimkabidhi mtuhumiwa kiasi hicho cha fedha taslimu na mtuhumiwa alimpatia mhanga karatasi nyeusi maarufu kama Makatoo na kumuelekeza akachanganye na dawa na kisha karatasi hizo zitageuka kuwa pesa.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji na hatimaye kumtia mbaroni mtuhumiwa. Aidha mtuhumiwa ameeleza kuwa amewahi kufanya matukio kama hayo mkoani Dodoma ambapo alitapeli fedha taslimu milioni kumi na tano.

MAFANIKIO YA KESI MBALIMBALI MAHAKAMANI KWA KIPINDI CHA MWEZI APRIL, 2022.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha mwezi April, 2022 limepata mafanikio katika kesi zilizokuwa zinaendelea kusikilizwa katika Mahakama zilizopo Mkoa wa Mbeya. Katika kipindi cha mwezi mmoja jumla ya kesi 59 za jinai na watuhumiwa 76 walipatikana na hatia na mahakama kutoa adhabu mbalimbali ikiwemo vifungo jela na faini.

Makosa ambayo walishitakiwa nayo ni pamoja na:- Mauaji, unyang’anyi, kuvunja nyumba na kuiba, wizi, kupatikana na bhangi na kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama barabarani.

Watuhumiwa 03 ambao ni 1. ALEX ROBERT, 2. ELIAS NIKO MUSHI @ MANGI na 3. GIDION NTULO walihukumiwa na mahakama kuu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mauaji mwaka 2017 ya VICTORIA MANASE aliyekuwa mfanyakazi wa Black Finance, Mkazi wa Airport Jijini Mbeya ambaye aliuawa kwa kukabwa shingoni na mwili wake kutupwa barabarani jirani na makaburi ya Isyesye. Katika uhalifu huo, walipora toka kwa marehemu fedha kiasi cha Tshs.2,040,000/=.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, tulifanya upelelezi, kuwakamata watuhumiwa na kisha kuwafikisha mahakamani, tulitoa ushahidi pamoja na wananchi kisha mahakama iliwatia hatiani watuhumiwa.

Imetolewa na:

[ULRICH O. MATEI – SACP]

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.