Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Wakazi wa jiji la Dodoma na Wilaya za Bahi, Chemba na Chamwino wanatarajia kuondokana na adha ya maji hivi karibuni baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB, kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 125. 2, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 289.34 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira-Dodoma.

Mkataba wa mkopo huo umesainiwa leo (tarehe 16 Mei 2022) jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa niaba ya  Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afika (AfDB), Dkt Patrician N. Laverley.

Dkt. Mwigulu alisema mradi huo unaokadiriwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi milioni 2, utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika miji hiyo unaotokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukame na ongezeko la watu baada ya idadi kubwa ya watu kuhamia mkoani humo.

 “Mradi huu umesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Dodoma lakini pia ni mradi ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ametamani kuona unataekelezwa, kusainiwa kwa mkataba wa mkopo huu kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi na upatikanaji wa maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya viwandani” alisema Dkt. Nchemba

Alifafanua kuwa mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na utahusisha ujenzi wa Bwawa la Maji la Farkwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji cubic metre 470, ujenzi wa mitambo ya kusafisha na kutibu maji yenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 128,000 kwa siku na mambo mengine kadha wa kadha.

Dkt. Nchemba aliiomba Benki hiyo kuangalia uwezekano wa kufikisha mradi huo kwenye maeneo mengine yaliyojirani na eneo la mradi ikiwemo Mkoa wa Singida, lakini pia kuweka matoleo ya maji kwa ajili ya shughuli za uzalishaji kama vile kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya mifugo, ufugaji wa samaki, itakayowawezesha vijana wengi kujiajiri.

“Mnapoanza utekelezaji wa mradi huu mkubwa muangalie pia maeneo jirani; mfano ukifika Bahi pembeni kidogo   kuna Manyoni Mashariki ambayo kuna shida kubwa ya maji na kuna mafuriko ya mara kwa mara; Kongwa kunapopakana na Chemba na Chamwino kuna shida kubwa ya maji pia, hivyo ni vyema kuyahusisha maeneo hayo kwenye mradi.” Alisisitiza Dkt Mwigulu

Dkt. Mwigulu alisema kuwa maelekezo ya Kiongozi wa Nchi, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ni kwamba miradi yote ya maji itakayotekelezwa hapa nchini kuanzia sasa iweze kuzalisha maji ya matumizi ya majumbani pamoja na kusaidia shughuli nyingine za uzalishaji kama vile kilimo, mifugo, uvuvi ili kuimarisha ustawi wa jamii kwa kujipatia kipato.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alirejea maombi ya Serikali kwa Benki hiyo kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) utakaoziunganisha na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo ili kusisimua biashara katika nchi hizo.

Alisema kuwa maombi hayo yamewasilishwa kwenye Benki hiyo na nchi hizo tatu na kwamba anaamini Mwakilishi huyo mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt. Patricia Laverley, atasimamia suala hilo ili mkopo huo pia upatikane kwa manufaa ya nchi hizo na Ukanda wa Afrika kwa ujumla.

Kwa Upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afika-AfDB Dkt. Patricia Laverley, alisema kuwa Benki yao iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi huo mkubwa wa maji Dodoma na kusaidia utekelezaji wa miradi mingine ambayo Benki hiyo ambayo Tanzania ni mwanachama, inatekeleza hapa nchini.

Aliahidi kuwa Benki yake itatoa fedha hizo kwa wakati ili wakazi wa maeneo yanayotarajiwa kufikiwa na mradi huo waondokane na adha ya maji lakini pia yawasaidie katika shughuli zao za kiuchumi zitakazo ongeza ajira na kuongeza kipato chao.

Dkt. Laverley alisema kuwa mkopo huo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 125.2 umefikisha kiasi cha fedha kilichowekezwa na Benki hiyo hapa nchini kufikia dola za Marekani bilioni 2.5, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 23 ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishaji, maji, na miundombinu ya barabara.

Kuhusu mkopo nafuu wa ujenzi wa reli ya kisasa, Dkt. Larveley, alisema kuwa maombi hayo yanafanyiwa kazi na Benki yake.

Mwisho.