Brela Yakusudia Kufuta Makampuni 5,676 Kwa Kushindwa Kukidhi Vigezo
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imetangaza kusudio la kufuta kampuni 5,676 kama awamu ya kwanza ambazo wanahisi hazifanyi biashara kwa kutimiza matakwa ya kisheria.
Kufanya hivyo kutasaidia daftari la kampuni kuwa na taarifa sahihi na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa majina ya kampuni.
Akizungumza na wanahabari Mei 27 jijini hapa, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema baadhi ya watu wamekuwa wakisajili na kushikilia majina na baadaye kuuziana.
"Tumegundua kuna hiyo tabia, watu wanauziana majina, mtu anashikilia mtu akilihitaji wanakubaluana ndiyo maana tumekuja na hili suala la kufuta ili watu waweze kuomba hayo majina," amesema.
Amesema Brela haitunzi makampuni mfu na badala yake yale yanayofanya kazi na watagundua hilo kwa kampuni husika kuwasilisha taarifa zake kila mwaka.
Amesema sababu zinazofanya kampuni kuonekana zimeshindwa kufanya kazi ni kutowasilisha taarifa za mahesabu ya mwaka kwa msajili, kukosa mtaji wa biashara, kuelemewa migogoro ya wamiliki kushindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa kuona hakuna namna ya kuendelea nayo kutokuwa na uelewa wa wakiliki na wakurugenzi.
Amesema kampuni hizo zitatangazwa katika magazeti na vyombo mbalimbali vya habari ili wamiliki waweze kujua kusudio hilo huku nakala ya barua itapelekwa katika anuani halisi za kampuni hizo
"Notisi hizi zitatolewa kwa awamu tatu, awamu mbili za kwanza zitakuwa siku 30 kila moja na ya tatu itakuwa siku 90 ili kutoa nafasi kwa wamiliki kuthibitisha kama kampuni zao zinafanya biashara," amesema.
Amesema notisi ya kwanza na pili itahusisha kampuni 5,284 zilizosajiliwa nchini na kampuni 392 zilizosajiliwa nje ya nchi.