Na Waandishi wetu, Dodoma
 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejipanga kuwajengea uwezo wa kazi watumishi wake ili kuwawezesha kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi.
 
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Jijini Dodoma
 
“Tumekuwa na kikao cha Baraza la Wafanyakazi kama ilivyo kwa mujibu wa Sheria, kikao kilijadili pamoja na mambo mengine, bajeti ya Wizara kwa mwaka mpya wa fedha 2022/2023, kuboresha utendaji kazi wa Wizara pamoja na maslahi ya watumishi.
 
“Katika masuala tuliyojadili leo katika kuboresja maslahi ya wafanyakazi ni pamoja na eneo la mafunzo ili kuendelea kuwajengeauwezo watumishi wetu wa kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo,” amesema Balozi Sokoine
Kwa upande wake Katibu wa TUGHE ngazi ya Taifa, Bw. Amani Msuya ameupongeza uongozi wa Wizara kwa kuyapa kipaumbele maslahi ya watumishi na kuwataka Watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na maarifa yote kwa maslahi mapana ya Taifa.
 
Naye Mwenyekiti wa TUGHE wa tawi la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Pilly Sukwa amesema kuwa kikao cha baraza kimejadili masuala ya Bajeti pamoja umuhimu wa kuboresha zaidi maslahi ya watumishi wa Wizara ili kuwaongezea morali ya kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa tija na ufanisi zaidi.
 
“Katika eneo langu mimi kama mwenyekiti wa TUGHE hapa Wizarani ni kuhakikisha kuwa maslahi ya watumishi ikiwemo mishahara na maslahi mengine yamezingatiwa. Ninaishukuru Wizara mambo yote haya yamezingatiwa wakati wa mkutano huu wa Baraza,” amesema Bi. Sukwa.
 
Baraza la Wafanyakazi wa Wizara limefanyika kwa lengo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2021/2022 na Makadirio ya Makisio ya Bajeti kwa Mwaka 2022/2023.
 
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo.