Wizara Ya Afya Na Serikali Ya Marekani Zajipanga Kuongeza Kasi Uchanjaji Wa Chanjo Dhidi Ya Uviko-19
Na.WAF,Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya, imejipanga kuongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika jamii kupitia msaada wa Dola za Marekani milioni 25 zilizotangazwa hivi karibuni kwenye kikao kilichofanyika Machi 3, 2022 kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi Samantha Jane Power Msimamizi Mkuu wa USAID.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Ummy Mwalimu wakati alipotembelewa na Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Waziri Ummy alianza kwa kumshukuru Balozi huyo baada ya Serikali ya Marekani ya Marekani kuipatia Tanzania Dola za Kimarekani Milioni 25 kupitia Mpango wa Serikali ya Marekani wa Global Vax ambao unalenga kuchangia kufikiwa kwa lengo la kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 70 ya watu wote duniani ifikapo Mwezi Disemba, 2022.
Waziri Ummy amesema fedha hizo zitatumika katika kuhamasisha makundi yaliyo hatari ya kuambukizwa UVIKO19 pamoja na makundi mengine yanayolengwa kufuatia kutofikiwa kwa malengo ya uchanjaji yaliyowekwa.
“Tutatumia ushawishi kwa viongozi wa ngazi zote na jamii kwa ujumla kupitia mikusanyiko na pia tunatarajia kuongeza idadi ya huduma za chanjo za mkoba karibu na jamii. Kwetu itakua ni sehemu nzuri ya kutoa elimu na kuhamasisha kuhusu chanjo”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Tanzania sasa ina chanjo ya UVIKO-19 inayoweza kuchanja watu takribani milioni 6 huku akiongeza kuwa fedha hizo zitasaidia kufikia lengo la kuchanja asilimia 70 ya watanzania.
Aidha, Waziri Ummy amemwambia Balozi Donald kuwa hivi sasa Wizara ya Afya imejikita katika kuimarisha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja kuboresha huduma za mama na mtoto na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Kwa upande wake Balozi huyo wa Marekani Dkt. Donald amesema Serikali yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyokuambukiza huku akisisitiza Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutoa elimu kwa jamii ili kujikinga na magonjwa.