Na. Mwandishi Wetu –Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekabidhi rasmi ofisi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. George Boniface Simbachawene ili kuendelea na majukumu katika ofisi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya ofisi hiyo Aprili 02,2022 iliyofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma Mhe. Balozi Chana alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumhamishia katika Wizara ya Maliasili na Utalii huku akiwashukuru watendaji na watumishi wote wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi chote alichohudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pia alitumia fursa hiyo kuendelea kuwakumbusha  watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao kwa kwa weledi na ufanisi katika kuratibu shughuli za serikali na kumpatia ushirikiano Waziri mpya aliyepewa kuhudumu katika nafasi hiyo ili kuendelea kuiletea Nchi maendeleo.

“Niwashukuru sana kwa ushirikiano ambao mmenipa, na mapokezi tangu nimefika tumekuwa tukishirikiano katika mambo mengi sana mnanishauri, mnanielekeza, mnaniongoza na tuendelee na moyo wa kuchapa kazi chini ya Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu,”Alishukuru Dkt. Pindi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe.  George Simbachawene  alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kutumikia nafasi hiyo huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na wepesi wa hali ya juu ili kuhakikisha Ofisi hiyo inaendelea kuwa ya mfano kwa shughuli inazozitekeleza huku akiwaomba watendaji kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayohitaji matokeo.

“Serikali ni timu moja uwe unafanya kazi yoyote ndani ya serikali wewe ni timu ile ile  kwa hiyo lazima  twende kulingana na maono ya viongozi wetu wakuu ili yakitimia basi watanzania wote wananufaika na Wizara hii ndiyo inabeba maana ya serikali lakini ofisi  hii ndiyo yenye matokeo lazima tufanye kazi kwa moyo na maono,”Alisema Mhe. Simbachawene.

=MWISHO=