Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikiliwa watu wawili kwa tuhuma za kujaribu kuharibu miundombinu ya Daraja la Tanzanite.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa watu hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, walikamatwa kwenye eneo hilo majira ya saa 10 alfajiri Aprili 2 mwaka huu wakijaribu kakata vyuma vya baadhi ya nguzo kwenye daraja.

Muliro ameeleza kuwa watuhumiwa hao wanahojiwa kwa kina na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi pale uchunguzi utakapokamilika.

Wakati huo huo kamanda Muliro amesema kwamba watu wengine 10 wanashikiliwa kwa kukutwa wakiokotoa vyuma chakavu chini ya daraja kwa ajili ya kwenda kuuza.

Amesema watuhumiwa hao wanaohojiwa ili kubaini sababu za uwepo wao eneo hilo na kuona kama wana uhusiano wowote na waliokamatwa wakijaribu kuharibu miundombinu ya daraja.

Daraja la Tanzania linalounganisha Babaraba za Barack Obama, Kenyatta na Toures lilianza kutumika Februari 1 mwaka huu, na lilizinduliwa rasmi Machi 24 na Rais Samia Suluhu Hassan.