Jeshi la Urusi limevitolea mwito vikosi vya Ukraine katika mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol kuweka chini silaha na kujisalimisha likionya kutakuwa na "taathira kubwa" baada ya muda uliowekwa kumalizika. 

Taarifa iliyotolewa na Jenerali Mikhail Mizintsev wa jeshi la Urusi imesema wapiganaji wa Ukraine wanapaswa kujisalimisha kuanzia asubuhi ya leo Jumapili na kuongeza kuwa wote watakaoweka chini silaha hawatashambuliwa. 

Kulingana na maelezo ya Urusi, wapiganaji wote wa mwisho wa Ukraine katika mji wa Mariupol wamezingirwa katika majengo ya kiwanda cha kufua chuma cha Azovstal na wanatakiwa kutoka mafichoni wakiwa na bendera nyeupe kabla ya saa saba mchana. 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema amezungumza kwa njia ya simu na viongozi wa Uingereza na Sweden kuhusu hali kwenye mji wa Mariupol anayosema kuwa ya hatari na kwamba Urusi inajaribu kumuangamiza kila mtu kwenye eneo hilo.